Mume aliyemkatakata mpango wa kando wa mkewe hadi kufa kufungwa
MAHAKAMA Kuu ya Nakuru jana ilimpata mlinzi mmoja na hatia ya kuua mpango wa kando wa mkewe aliyemfumania na mke wake huyo katika eneo la Kiamunyekeni, Kaunti ya Nakuru.
Cyrus Kipng’eno Rono ambaye ni mlinzi wa usiku alikuwa amempigia simu mkewe lakini haikuwa ikipokelewa.
Rono alienda nyumbani saa tatu usiku na alipobisha mlangoni, mkewe alionekana kuchanganyikiwa na kutojielewa akiufungua.
Alishikwa na mshtuko alipoona viatu vya mwanamume mshukiwa. Alifululiza na kupekua hadi alipompata chini ya kitanda.
Mshukiwa kwa jina Moody Awori alikuwa nusu uchi naye mlinzi huyo akamwangushia kipigo kikali kisha kumkata kwa upanga.
Awori alijeruhiwa vibaya na akipambania uhai wake, Rono alienda kuripoti kuhusu kisa hicho katika kituo cha polisi cha Lanet.
Akiwa ameandamana na polisi, alirejea na kumpata Awori akiwa amefariki kisha akakamatwa, na polisi kuichukua silaha yake.
Kortini, Mwanapatholojia wa Serikali, Dkt Titus Ngulungu alithibitisha Awori aliaga dunia kutokana na majeraha ya kupigwa kwa kifaa butu na kukatwa.
Mkewe Rono alikataa kuwa shahidi kwenye kesi hiyo lakini awali alikuwa ameandikisha taarifa kwa polisi kuhusu tukio hilo.
Rono alidai alikuwa akijilinda, akidai Awori alikuwa amejaribu kumvamia.
Hata hivyo, Jaji Samuel Mohochi alipuuza utetezi wake akisema jinsi ambavyo mwili wa Awori ulipatikana umelowa damu, lazima alikuwa amepigwa vibaya na mshtakiwa.
Ripoti ya kuhukumiwa kwa Rono itaandaliwa kisha ataambia atatumikia kifungo cha muda upi gerezani.