Mumias Sugar yalaumiwa kwa wizi wa miwa Magharibi ya Kenya
MAAFISA wa kampuni ya kutengeneza sukari ya Mumias (MSC) walijaribu kuiondolea lawama kuhusu madai kuwa kampuni hiyo inaendeleza wizi wa miwa mashambani, uovu unaoitishia kufungwa kwa viwanda vingine vya kutengeneza sukari.
Wasimamizi wa kampuni tano za sukari wamelaumu usimamizi wa kampuni ya Mumias kwa “kuvuna” mahala ambapo “hawakupanda”.
Hii ndiyo maana maafisa wa MSC walikuwa na wakati mgumu kuelezea ni kwa nini wanashukua miwa isiyotimu miezi 10 na iliyopandwa katika mashamba yaliyokodiwa na kampuni nyingine za sukari.
Haya yalijiri wakati wa kikao cha kukusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu kero ya wizi wa miwa mashambani na uagizaji wa sukari kutoka ng’ambo, maovu yanayoathiri sekta ya sukari katika eneo la Magharibi mwa Kenya.
Wakulima walioshiriki mkutano huo ulioitishwa na Kamishna wa Ukanda wa Magharibi Irungu Macharia, walitoka Kaunti za Busia, Kakamega na Bungoma.
Wawakilishi wa kampuni zote kutoka Magharibi mwa Kenya pia walihudhuria wakidai kuwa kampuni ya Mumias inaua sekta ya sukari nchini kwa kuendeleza uvunaji wa miwa changa.
Bi Monica Mungala, mkulima na diwani maalumu kutoka Busia aliitaka Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) na maafisa wakuu wa usalama kuchukulia hatua kampuni za miwa zinazoendeleza wizi wa miwa.
“Kampuni hizi zote za sukari zinaelekeza kidole cha lawama kwa kampuni ya Mumias. Wote hawawezi kuwa wanadanganya. Hii ina maana kuwa kuna shida kubwa ambayo inapasa kushughulikiwa kuokoa sekta hii ya sukari,” akasema Bi Mungala.
Bi Mungala aliitaka mamlaka ya AFA kueleza ikiwa kuna kampuni ya sukari katika eneo la Magharibi mwa Kenya ambayo haiwezi kuadhibiwa.
“Kinaya ni kwamba kampuni hii ya sukari ya Mumias ambayo inatuhumiwa kuiba miwa changa, ndiyo yenye miwa ya umri wa zaidi ya miezi 20 katika mashamba yake. Mbona isivune miwa yake iliyokomaa na itoe nafasi kwa miwa changa iweze kukomaa?” akauliza Bw Mungala.
Simon Oduki, ambaye ni mkulima kutoka Busia, alitaka kujua sababu ya kampuni ya sukari ya Mumias kuvuna miwa isiyokomaa ilhali hamna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yake.