• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Mung’aro abadili nia kuhusu ‘kumpelekea Kindiki’ miili ya Shakahola

Mung’aro abadili nia kuhusu ‘kumpelekea Kindiki’ miili ya Shakahola

NA WACHIRA MWANGI

GAVANA wa Kilifi, Gideon Mung’aro, amebadili uamuzi wake wa kuhamisha miili ya waathiriwa wa Shakahola kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Malindi kwenda Nairobi.

Mabadiliko hayo yalijiri baada ya ukaguzi wa kontena zinazohifadhi miili hiyo katika kituo hicho, uliofanywa kwa ajili ya kujiandaa kwa uhamisho wao uliopangwa Jumatatu.

Alhamisi iliyopita, Gavana Mung’aro alitoa makataa kwa serikali ya kitaifa, akitaka kuondolewa kwa miili hiyo ifikapo Jumatatu.

Alitishia kuhamisha maiti hayo kwenda Nairobi kutokana wa gharama kubwa ya umeme na harufu mbaya inayotoka kwa miili hiyo, akidai kuwa inawaathiri wagonjwa wengine hospitalini.

Hata hivyo, msimamo wa Gavana Mung’aro ulibadilika Jumapili alipofanya ziara ya ghafla katika kituo hicho.

Baada ya mkutano mfupi na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai wa DCI, Bw Martin Nyuguto, Gavana Mung’aro alifanya ukaguzi wa vyombo hivyo na kutangaza njia mpya.

Alifichua makubaliano na maafisa wa uchunguzi wa jinai wa DCI kuharakisha kutoa miili kwa ajili ya vipimo vya DNA mara tu itakavyowezekana.

“Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki aliahidi kutangaza eneo Shakahola kwa ajili ya kaburi la pamoja la miili iliyobaki. Wakati huo utakapofika, tutaweza kuhamisha miili,” Gavana Mung’aro alisema.

Aidha, Gavana Mung’aro alifafanua dhana potofu kuhusu vyombo hivyo, akisema kuwa vinatumia gesi, sio umeme, na kwamba hakuna harufu inayotoka kwa miili hiyo.

Aliweka wazi kwamba harufu yoyote katika eneo la chumba cha kuhifadhi maiti ilitokana na miili mingine iliyohifadhiwa katika kituo cha kaunti.

Kukiri kushughulikiwa kwa bili ya umeme iliyopatikana kabla ya kubadilisha kutumia gesi, Gavana Mung’aro aliitaka serikali kuu kuharakisha mchakato wa kufanikisha upimaji wa DNA na kutolewa kwa miili kwa jamaa.

“Tunawaomba watu wote ambao wanajua kuwa jamaa zao walikwenda Shakahola kujitokeza na kutoa sampuli za DNA bila hofu,” alisema.

Miili isiyodaiwa na jamaa itazikwa katika kaburi la pamoja katika sehemu iliyotengwa ya msitu wa Shakahola.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa jinai wa DCI Nyuguto alisema miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa vizuri, akisisitiza umuhimu wao kama ushahidi katika kesi inayoendelea ya mauaji na umuhimu wa mchakato wa haki kabla ya kutoa miili hiyo.

Mabadiliko ya msimamo wa gavana yanathibitisha juhudi zinazoendelea za kushughulikia janga la Shakahola kwa hisia na ufanisi, kipaumbele kikiwa ni taratibu za kisheria na mahitaji ya familia zilizoathiriwa.

  • Tags

You can share this post!

Israel yavamia Al Jazeera baada ya amri ya kufungwa kwa...

Raila achomoa kucha na kushambulia serikali baada ya kimya...

T L