Habari MsetoSiasa

Mungatana akiri kupoteza hela lakini sio kwa waganga

October 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

ALIYEKUWA mbunge wa Garsen, Bw Danson Mungatana hatimaye ameelezea masaibu yake baada ya kupoteza mamilioni ya fedha kwa walaghai.

Bw Mungatana, hata hivyo, alikanusha madai kwamba alihadaiwa na waganga waliomwahidi kumzalishia fedha awe bilionea.

Mbunge huyo wa zamani aliyekuwa akihutubia wanahabari jijini Nairobi alisema alikuwa mwathiriwa wa utapeli uliohusisha wafanyabiashara mashuhuri wa humu nchini na raia wa kigeni.

Alisema matapeli hao walianzisha mradi wa uwekezaji uliohusisha ununuaji na uuzaji wa mafuta. Matapeli hao waliwataka mabwenyenye wa humu nchini kuwekeza katika mradi huo kwa kuwapa ahadi kwamba wangelipwa kiasi kikubwa cha faida.

“Mara ya kwanza tulipewa mgao wa faida, mara ya pili pia tukapewa mgao huo. Mara ya tatu raia hao wa kigeni walitoweka na fedha zetu,” akasema Bw Mungatana ambaye pia amewahi kuwa waziri msaidizi wa Huduma za Matibabu.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari, Bw Mungatana alitapeliwa Sh76 milioni.

Lakini yeye jana alikataa kufichua kiasi cha fedha alizopoteza na badala yake akasema kuwa “nilipoteza mamilioni ya fedha.”

Raia wa kigeni waliotambuliwa kwa majina ya Abdoulaye Tamba, Abdalla Tamba – wote raia wa Chad pamoja na Anthony Mwangangi ambaye ni dereva wao tayari wanazuiliwa rumande baada ya mahakama kuagiza wazuiliwe kwa siku 15 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi wao.

Washukiwa hao walinaswa na maafisa wa upelelezi katika eneo la Brookside Drive mtaani Westlands, Nairobi ambapo walipatikana na noti ghushi Sh1 bilioni.

“Polisi walinasa washukiwa mnamo Septemba 28 na wakawataka Wakenya ambao wametapeliwa kujitokeza na kuwatambua washukiwa hao. Nilimtambua Abdalla Tamba ambaye ni mmoja wa watu walionitapeli kwa njia tofauti sana na sio uchawi kama ilivyodaiwa,” akasema Bw Mungatana.

“Sikutaka kuwa bilionea kwa siku moja namna inavyodaiwa. Mama yangu hakunifundisha kutafuta utajiri wa haraka kwa kutumia njia za mkato. Nimekuwa mchapakazi tangu nilipozaliwa,” aliongeza.

Wakili huyo alishtumu baadhi ya vyombo habari kwa ‘kunifanya kuonekana mjinga baada ya kutapeliwa’.

“Ni kweli nilisomea katika shule ya Upili ya Alliance na nikafanya vyema katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Kwa sasa nasomea Uzamifu (PhD). Lakini uhalifu huo unaweza kutokea kwa yeyote. Uhalifu hauheshimu digrii au masomo,” akasema.

Kulingana na Bw Mungatana watu mbalimbali maarufu walinaswa na mtego wa matapeli hao lakini hawajaripoti kwa sababu wanaogopa kukejeliwa.