• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Murkomen: Afisi yangu haihusiki na uchunguzi wa ndege iliyoua Ogolla

Murkomen: Afisi yangu haihusiki na uchunguzi wa ndege iliyoua Ogolla

HILARY KIMUYU NA LABAAN SHABAAN

WAZIRI wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema wizara yake haitachunguza usalama wa ndege ya kijeshi iliyomuua Mkuu wa Idara ya Jeshi Francis Ogolla.

Hii ni baada ya kutangazwa kwa jopokazi la kuchunguza ajali za ndege siku chache baada ya helikopta ya kijeshi kuanguka na kuua maafisa 10 wa kijeshi.

Bw Murkomen alisema kuwa afisi yake itahusika kuchunguza ajali za ndege za usafiri wa kiraia.

“Tumeshuhudia ajali ndogo za ndege kama ile iliyotokea katika Angatua ya Wilson. Kama idara ya uchukuzi, hatuchunguzi ndege za kijeshi,” alisema.

Bw Murkomen alirejelea kauli ya Rais William Ruto siku ya mazishi ya Jenerali Ogolla Jumapili.

Rais alisema upelelezi wa ajali za ndege za kijeshi utafanywa upesi na Idara ya Ulinzi na matokeo kuwekwa wazi kwa umma.

“Ni muhimu kujua kwamba Wizara ya Uchukuzi ina jukumu la kisheria la kuchunguza ajali zinazohusisha ndege za kibinafsi na za kibiashara,” aliendelea Bw Murkomen.

Juma lililopita wizara hiyo ilitangaza jopo la wanachama saba kuchunguza ajali zote za ndege zilizofanyika miaka mitatu iliyopita.

Timu hiyo inaongozwa na Rubani  Peter Maranga na inatarajiwa kutoa mapendekezo ya kuzuia ajali angani ili kuimarisha usalama.

Kikosi hicho pia kinahusisha Rubani Nduati Herman Njama, Luteni Kanali Mstaafu Mike Mulwa, Ephantus Kamau, Rubani Valentine Wendoh, Rubani Martin Lunami na Brenda Mwango.

Jopo hili limepewa miezi mitatu kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti kwa waziri.

Kadhalika, watatathmini ripoti za awali za ajali zinazohusisha ndege zilizosajiliwa Kenya.

Ripoti hizi ziliwasilishwa na Jamhuri ya Sudan Kusini na Somalia kuhusu ajali zilizotokea miaka 5 iliyopita.

  • Tags

You can share this post!

Demu awaka kupata picha za mume akila bata na manyanga...

Misa ya ukumbusho wa Jenerali Ogolla yaahirishwa

T L