Mutava Musyimi: Nilinyimwa kura kwa kupinga ugawaji wa ardhi ya Mwea
Na CHARLES WANYORO
ALIYEKUWA Mbunge wa Mbeere Kusini amedai kuwa alinyang’anywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8 kwa sababu alipinga ugawaji wa ekari 44,000 ya ardhi katika mpango wa makazi ya Mwea.
Kasisi Mutava Musyimi aliyewania kiti hicho kwa kama mgombeaji wa kibinafsi alisema ana ushahidi kwamba alishinda Bw Geoffrey King’ang’i wa Jubilee aliyetangazwa mshindi.
Kulingana na yaliyotolewa na Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw King’ang’i alipata kura 18,028 huku Musyimi akiwa wa pili kwa kura 16,854. Bw Genesio Mugo alikuwa wa tatu kwa kujishindia kura 6,899 akifuatwa kwa karibu na Nerbert Mugo aliyepata kura 6857.
Wagombeaji wengine, wakiwemo aliyekuwa Waziri wa Vijana kaunti ya Embu Emily Thaara, mfanyabiashara wa Nairobi Kamau Nyutu, Bw Atanasio Njue, Bw Erusmus Mwangi na Bi Sarah Mwige walipata chini ya kura 4,000 kila mmoja.
Akiongea katika hafla ya mazishi ya Kennedy Muvevi Mutua alifariki baada ya kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano kuhusu ardhi hiyo, Bw Musyimu alisema alipokonywa ushindi kwa sababu ya msimamo wake kuhusu ardhi hiyo. Alisema aliamua kutowasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Kang’ang’i kwa sababu hakuwa na hakika kwamba angepata haki “kwa sababu ya mzozo kuhusu ardhi hiyo”.
“Mlipiga kura mnamo Agosti 8 ambapo mlinichangua kama Mbunge. Lakini udanganyifu uliofanyika na nikapokonywa ushindi. Huo ndio ukweli. Nilisema sitafuatilia suala hilo kortini kwa sababu singepata haki kwa sababu ya nilipinga uganyaji wa ardhi katika mpango wa makazi ya Mwea,” Bw Musyimi akawaambia waombolezaji.
Mbunge huyo wa zamani alifananisha mauaji ya hivi majuzi wa wakazi wa mpango wa makazi wa Mwea na mauaji ya kinyama ya babake, Mzee Stephen Kisilu, mnamo 1977.
Bw Musyimi alisema babake aliuawa kwa sababu ya msimamo wake kuhusu ugawanyaji wa ardhi katika eneo la Riakanau.
Mpaka sasa wakazi wa eneo hilo hawajapewa vyeti vya umiliki wa ardhi.
Hata hivyo, Bw Musyimi alisema familia yake ilikubali kuwasamehe wauaji hao na itaandaa hafla ya ukumbusho kwa heshima yake mnamo Julai mwaka huu.