Mutua 'azima' matumaini ya seneta kuhusu Sh390 milioni
Na KITAVI MUTUA na MARY WANGARI
MZOZO unatokota kati ya Gavana wa Kaunti ya Machakos Dkt Alfred Mutua na Seneta Boniface Kabaka kuhusu malipo ya Sh390 milioni zinazodaiwa na seneta huyo huku gavana akisisitiza hataidhinisha kamwe malipo hayo.
Kulingana na Seneta Kabaka, shirika lake la sheria lilifanya kazi ya kukusanya ada za ardhi kutoka kwa Taasisi ya Uchunguzi kuhusu Mifugo (ILRI) –ambalo ni shirika la utafiti lisilo la kiserikali ambalo lilifanya makao kwenye ardhi ya Kapiti eneo la Machakos, yenye thamani ya mabilioni.
Alisema alimaliza kazi hiyo kuambatana na maagizo ambapo ameelekea kortini akitaka kulipwa ada yake kwa kutoa huduma za kisheria alizotoza Sh390milioni
“Ndio, nimeenda kortini kuishinikiza serikali ya kaunti kulipa ada yangu. Huduma zangu za kisheria hazikuwa za bure hivyo ni sharti walipe,” seneta alieleza Taifa Jumapili.
Hata hivyo, Gavana Mutua alisema Bw Kabaka alipatia kazi shirika lake binafsi kwa njia ya udanganyifu na kisiri ya kukusanya ada ambazo hazikuwepo kutoka kwa ILRI, alipokuwa akihudumu kama mtaalamu na mshauri wa masuala ya kisheria katika kaunti hiyo.
“Ni vipi afisa wa umma anaweza kuteua shirika lake binafsi la sheria kufanya kazi ya serikali? Huu ni udanganyifu wazi na matumizi mabaya ya afisi,” alisema Dkt Mutua akisisitiza kuwa hataruhusu malipo hayo.
Kutoifahamu
Aidha, gavana huyo alisema hakufahamu kuhusu kazi hiyo ya kisheria na alijua tu wakati seneta alipowasilisha madai ya kutaka malipo.
“Alijipatia kazi hiyo kisiri na alipaswa kujua kwamba ILRI ni shirika la kimataifa ambalo halitozwi ada za ardhi kuambatana na maafikiano ya kimataifa na kanuni,” alisema gavana.
Bw Mutua pia alimtaka Bw Kabaka anayejiandaa kumrithi 2022, kuonyesha ushahidi wa hela anazodai alikusanya kwa niaba ya serikali ya kaunti kutoka ILRI maadamu hakuna hata senti iliyopokewa na hazina ya kaunti Machakos.
Mzozo kuhusu malipo hayo sasa umegeuka uhasama wa kisiasa kati ya Gavana Mutua na Seneta Kabaka, waliokuwa marafiki wa karibu katika hatamu ya kwanza ya Dkt Mutua afisini kiasi cha kumteua seneta huyo kama mkuu wa sheria katika kaunti na mshauri wake kisheria kuanzia 2014 kabla ya kutofautiana.
Bw Kabaka amekuwa akimshutumu Dkt Mutua dhidi ya kuongoza serikali fisadi huku kisa kipya zaidi kikiwa walipojibizana hadharani wiki iliyopia katika shamba la maskwota la Muli.