• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Muuzaji chang’aa aliyewapiga machifu wanne aachiliwa kwa dhamana ya Sh25,000 pesa taslimu

Muuzaji chang’aa aliyewapiga machifu wanne aachiliwa kwa dhamana ya Sh25,000 pesa taslimu

Na MARY WANGARI

MAHAKAMA moja Kiambu mnamo Alhamisi imemwachilia kwa dhamana ya Sh25,000 pesa taslimu mwanamume aliyewapokeza kichapo cha mbwa machifu wanne waliokuwa wakijaribu kumkamata katika kibanda cha kuuzia chang’aa.

Iliripotiwa kuwa muuzaji pombe huyo aliwatandika bila huruma machifu hao wanne: Peter Gachuhi, Robert Muigai, Samuel Mburu, na Robert Muiruri mnamo Desemba 30, 2019, walipoenda kumkamata katika soko la Wangige.

Kulingana na Chifu wa Wangige, Samuel Mburu, maafisa hao wa umma walilazimika kukimbizwa hospitalini kwa matibabu kufuatia kichapo hicho ambapo baadaye waliandikisha ripoti katika kituo cha polisi cha Kibiku.

“Tulimfumania na tukachukua hatua ya kumkamata ambapo alizua fujo. Alinigonga usoni na kwenye mdomo. Wenzangu pia walishambuliwa,” alisema Mburu.

Alieleza kwamba mshukiwa amekuwa akiachiliwa huru kila mara hata baada kukamatwa.

“Huyu ni mwanamme ambaye tumekamata mara kadha lakini mahalakama humwachilia huru kila mara kwa dhamana ya pesa taslimu ya kiwango cha chini. Tunamfahamu na huendesha shughuli zake kutoka Soko la Wangige,” alisema.

Akimtetea mshukiwa wakati wa kusikizwa kwa kesi, wakili wa mshukiwa aliiomba korti kumwachilia huru mshtakiwa kwa kuwa ndiye aliyekuwa tegemeo la pekee la familia yake.

Mahakama ilimwachilia huru mshukiwa kwa dhamana huku akimwamrisha awe akiripoti katika vituo vya polisi kila mara anapohitajika kufanya hivyo ili kuhojiwa.Aidha, mshukiwa alionywa dhidi ya kutishia au kuwashambulia wahasiriwa au mashahidi katika kesi hiyo.

You can share this post!

Msongamano vituo vya mabasi Mombasa wageni wakirudi...

UANDISHI: Mathias Momanyi ni mwandishi mahiri wa vitabu vya...

adminleo