Habari Mseto

Maji ya mafuriko yasababisha kadhia Thika

December 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Athari za mvua ya mafuriko

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa eneo la Kisiwa, Thika wanaiomba serikali kuwasaidia hii ikiwa ni baada ya maji maenge kuzingira baadhi ya makazi.

Hali hiyo inashuhudiwa kufuatia mvua inayoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Mengi ya majengo ambayo hayajatengenezewa mikondo yamezingiriwa na maji, wakazi wakikosa namna ya kutoka au kuingia. Isitoshe, maji hayo yanayaweka katika hatari ya kuporomoka.

“Ni rahisi msingi wa nyumba kufanywa dhaifu, ikiporomoka itatuletea madhara,” mkazi akaambia Taifa Leo.

Taswira sawa na ya Thika pia imeshuhudiwa eneo la Zimmerman, ambapo majengo kadha yamezingirwa na maji.

Ni hatari kwa maisha ya wakazi, hali hiyo ikihofiwa kuweza kusababisha maafa na mkurupuko wa maradhi kama Kipindupindu.

Wadudu hatari aina ya mbu na wanaosababisha Malaria hujificha kwenye mazingira yenye maji yaliyotapakaa na mimea iloyomo.

Mvua ya mafuriko inayoendelea kushuhudiwa nchini hasa majira ya jioni, maeneo yaliyoathirika zaidi ya watu 100 wameripotiwa kufa maji. Siku kadha zilizopita, watu wasiopungua 50 kaunti ya Pokot Magharibi walizikwa na kufariki kupitia maporomoko ya udongo.

Maafa pia yameripotiwa eneo la Ruiru, na Kiambu.