• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mvulana wa miaka 14 azuiliwa kwa madai ya kunajisi makinda mawili

Mvulana wa miaka 14 azuiliwa kwa madai ya kunajisi makinda mawili

NA TITUS OMINDE

MAPEMA wiki, hii mahakama ya Eldoret iliamuru kuzuiliwa kwa mvulana mwenye umri wa miaka 14 anayeshukiwa kunajisi watoto wawili akisubiri kutafutiwa wakili wa kumwakilisha.

Mshukiwa huyo anadaiwa kunajisi mvulana na msichana wa umri wa miaka 8 na 10, mtawalia.

Kulingana na afisa wa uchunguzi kutoka kituo cha polisi cha Ainaptich, mshukiwa ana rekodi ya kunajisi watoto katika mtaa wao, ilidaiwa kuwa alikuwa amenajisi watoto wengine sita katika mtaa huohuo.

Akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Rodgers Otieno, mtoto huyo hakuruhusiwa kujibu mashtaka kutokana na matakwa ya kisheria kwamba lazima awe na wakili wa kumwakilisha katika kesi hiyo.

Hakimu alimwambia wakili wa serikali, Meshack Rop, kwamba kuna haja ya kuhakikisha mtoto huyo anawakilishwa na wakili kabla ya kusomewa mashtaka.

Wakili wa serikali alikubaliana na hakimu.

Bw Otieno aliamuru afisa mtendaji wa mahakama hiyo kupitia kwa Kamati ya Watumiaji wa Mahakama (CUC) kusaidia mtoto huyo kupata wakili wa kujitolea.

Mtoto huyo alisababisha kicheko mahakamani alipomweleza Hakimu kuwa yuko raha kurudishwa katika kituo cha uokoaji cha Eldoret Rescue Centre akisema maisha katika kituo hicho yalikuwa mazuri.

“Unataka kurudi kituoni hadi urudishwe Ijumaa?” Hakimu aliuliza huku mtoto akijibu kwa kujiamini, “ndio”.

Hakimu aliamuru mtoto huyo azuiliwe katika kituo cha uokoaji cha Eldoret kwa siku tano akisubiri kupatikana kwa wakili wa kumwakilisha.

Mtoto huyo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 23 na 24, 2024 katika mtaa wa Jerusalem Estate katika Kaunti Ndogo ya Moiben, Eldoret.

Mahakama pia iliagiza mtoto huyo apelekwe hospitalini kwa uchunguzi wa umri ili kubaini umri wake kabla ya kufunguliwa mashtaka.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 12.

  • Tags

You can share this post!

Ukatili: Mwanaharakati wa LGBTQ alinyongwa hadi kufa  

Viongozi wa Kiislamu wahimiza serikali kutendea haki...

T L