Mvurya abainisha mpango wake Kwale kukabili Covid-19
Na WINNIE ATIENO
GAVANA wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya amesema madereva 11 ambao sampuli zao zilichukuliwa na vipimo vikabainisha wana Covid-19 eneo la mpakani waliambiwa wasalia nchi jirani ya Tanzania.
Amesema serikali ya kaunti yake itaendelea kuweka mikakati kabambe kukabiliana na janga hilo hatari.
“Tunaendelea kujitahidi kukabiliana na Covid-19. Jumapili tuliwaambia madereva 11 wa malori kutoka Tanzania wasalie upande wao baada ya kupatikana na virusi vya corona,” amesema Mvurya.
Amefichua pia kwamba serikali yake ya kaunti imepata mgonjwa mwingine mwenye virusi hivyo eneo la Kombani.
Kulingana na gavana huyo mgonjwa huyo kutoka Mombasa alipatikana na virusi hivyo baada ya kupimwa.
Amesema anaendelea kutengwa katika kituo maalum cha wagonjwa wa Covid-19 huko Msambweni na waliotangamana naye wakiwekwa karantini.
“Kadri visa vinayoendelea kuongezeka inafaa tuwe makini hususan na majirani zetu hasa wale wanaotumia njia za mikato kuingia Kwale. Lazima tushirikiane kumaliza janga hili,” akasema.
Wakati huo huo gavana huyo amesema kamati ya kupambana na virusi hivyo, imetangaza kuruhusiwa kwa mikahawa ili kuhudumia wateja wao.
Hata hivyo, amesisitiza ni sharti wafuate maagizo na taratibu maalum ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.
“Tumetangaza kufunguliwa kwa hoteli lakini wafanyakazi wote watapimwa. Tutatoa huduma za bure za kupima wafanyakazi wafikao watano wa kila mkahawa. Lakini hoteli ambazo zitahitaji wafanyakazi zaidi ya watano zitalipia Sh500 kwa kila mwajiriwa,” akabainisha.
Hata hivyo wafanyakazi hao watatakiwa kupimwa kila baada ya siku 21.
Amesema idara ya afya ya umma itatoa mwongozo wa namna wawekezaji wa sekta hiyo wataendesha shughuli zao.