Habari Mseto

Mvurya awataka wakazi wa Mwereni waache kuuza ranchi kiholela

August 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kwale Salim Mvurya amewaonya wakazi wa Mwereni dhidi ya kuuza mashamba makubwa; yani ranchi, huku wale waliokuwa wameuza wakishurutishwa warejeshe fedha hizo.

Bw Mvurya alilalama kwamba wakazi wanauza mashamba ya ukubwa wa ekari 100 kwa kitita cha Sh6,000 pekee.

“Inasikitisha kugundua kwamba shamba la ekari 100 limeuzwa kwa Sh6000. Hii tabia ya kiajabuajabu ikome mara moja. Tabia hiyo sasa imezua taharuki miongoni mwa jamii zinazoishi sehemu hiyo,” alisema Bw Mvurya.

Wiki iliyopita Bw Mvurya alizuru eneo hilo kuthathmini visa vya kuuza mashamba huku akionya wakazi wa jamii za Waduruma, Wamasai, Wakamba miongoni mwa zingine zinazokaa sehemu hiyo kuishi kwa amani na kuacha kuzozana.

Mbunge wa eneo hilo Bw Khatib Mwashetani, mwakilishi wa wadi Manza Beja na maafisa wa serikalini walizuru eneo hilo ili kusaka mwafaka.

“Tumeamua kwa kauli moja kwamba wale wanaoendelea kuuza mashamba waache mara moja. Ranchi ya Mwereni haiuzwi. Kama uliuza shamba lako tafadhali regesha fedha hizo kwa mnunuzi wako,” alisisitiza Bw Mvurya.

Aliwataka wakazi kuishi kama ndugu akiongeza kuwa mpango wa kugawanya ranchi hiyo utatekelezwa.

Alisema atafanya kikao na viongozi wa wilaya ya Lunga Lunga wiki hii ili kutafuta suluhu la suala la mashamba.

“Serikali ya kaunti yangu itahakikisha wakazi wote wanapata hatimiliki. Lakini tunawahisi mtupashe kuhusu wale watu wabinafsi ambao wanauza mashamba yao ili tuchukue hatua kali za kisheria. Niliwaambia na ninawaambia tena; msiuze mashamba yenu,” alisisitiza.