• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Mvurya awavulia kofia kina mama Pwani kwa bidii yao kiuchumi

Mvurya awavulia kofia kina mama Pwani kwa bidii yao kiuchumi

NA MKAMBURI MWAWASI

WAZIRI wa Madini na Uchumi wa Baharini Salim Mvurya amezitaka jamii kuunga mkono kina mama, akisema wanatekeleza wajibu muhimu katika ukuaji wa kiuchumi wa eneo la Pwani.

Akiongea jijini Mombasa, Bw Mvurya alisema wanawake wa Pwani wamechukua majukumu mengi ya kuimarisha familia zao na jamii kwa ujumla.

“Kina mama wamejitwika majukumu ya uchumi wa baharini ili kuweka chakula kwa meza za familia zao. Hata hivyo, michango yao mara nyingi huwa haijatambuliwa wala kuthaminiwa,” alisema Bw Mvurya.

Waziri huyo aliwataka wanaume kuwaunga mkono wanawake katika shuhuli zao za kila siku, akishauri kwamba maisha ya sasa yanahitaji ushirikiano wa waume kwa wake.

Bw Mvurya aliongeza kwamba wanawake ni mojawapo ya wanaotoa maamuzi makuu katika sekta mbalimbali kama vile uvuvi, ufugaji wa samaki, uhifadhi wa bahari na utalii.

“Kuhusika kwao sio tu muhimu kwa kufikia usawa wa kijinsia lakini pia kwa kuongeza uwezo wa kiuchumi wa Pwani na taifa kwa ujumla,” Bw Mvurya aliongeza.

Alitaja changamoto zinazowakumba kina mama katika sekta ya uchumi wa baharini ikiwa ni pamoja na upatikanaji mdogo wa rasilimali, huduma hafifu za ufadhili wa kifedha, mafunzo duni, na kukosekana kwa wanawake wengi katika majukwaa ya kufanyia maamuzi muhimu.

Aliongoza kwamba kanuni za kitamaduni na kijamii pia zinazuia ushiriki wao na kuzuia uwezo wao wa kutumia kikamilifu fursa zilizoko katika sekta hii.

“Ni lazima kukabili vikwazo hivi na kuunda mazingira wezeshi ambayo yanawawezesha wanawake kustawi katika uchumi wa samawati au uchumi wa naharini,” alisema.

Alisema ni muhimu kina mama kupata elimu, ujuzi, vifaa vya mikopo, fursa za uongozi na kuiomba jamii kupinga dhana potofu za kijinsia na kuwahusisha kina mama katika ngazi zote za kufanya maamuzi.

“Nimejitolea kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika sekta hii. Serikali ya Kenya imetekeleza mipango mbalimbali ya kusaidia wanawake katika sekta hii,” akafichua.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti ya Kilifi yatenga Sh39m kwa basari muhula wa pili

MWANAMIPASHO: Sina chuki, ila hapa kwa TID mwanishangaza

T L