Habari Mseto

Mvuvi Mkenya aogelea kilomita tano kukwepa wanajeshi wa Uganda

January 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

GAITANO PESSA Na PETER MBURU

MVUVI mmoja wa Kenya amesema kuwa Jumanne aliponea kifo kwa kuruka kutoka meli, kisha kuogelea umbali wa zaidi ya kilomita tano, wakati alipokumbana na wanajeshi wa Uganda waliojihami alipokuwa akivua samaki karibu na ufuo wa Majanji.

Bw Ben Wandera kutoka kijiji cha Buduong’I, eneo la Funyula kaunti ya Busia alisema kuwa tukio hilo la saa saba usiku liliokoa maisha yake, kwani wenzake watatu walikamatwa na kuzuiliwa katika kambi ya wanajeshi Uganda.

“Walituvamia wakati tulikuwa tukitumbukiza nyavu za kutaga samaki na kuanza kutupiga. Walikuwa kama maafisa kumi waliojihami kwa bunduki na panga. Wenzangu waliokuwa mbele ya mashua waliumizwa lakini maafisa hao waliponikaribia nilinyakua gwanda la kuogelea na kuruka ziwani,” akasema Bw Wandera.

Lakini jamaa huyo alisema kuwa licha ya kudhani kuwa baada ya kuhepa wangechanganyikiwa na kuwaacha wenzake, alipokuwa akiogelea alisikia vilio vya wenzake kutokana na kichapo walichokuwa wakipokea.

“Hata hawakushughulika kunifuata, lakini nikiogelea nilikuwa nikisikia vilio vya wenzangu,” akasema.

Mvuvi huyo alisema kuwa wamekuwa wakivamiwa mara kwa mara na maafisa kutoka Uganda, akitoa wito kwa serikali ya Kenya kudhibiti hali.

“Wavuvi wa Kenya wamefanywa mateka na wanajeshi wa Uganda katika ziwa Victoria. Ni kama serikali imetupilia watu wake. Wanajeshi wa Uganda hutuchapa na kutuibia,” akasema.