• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mwaka Mpya: Wahuni 6 wavamia na kujeruhi wanakijiji

Mwaka Mpya: Wahuni 6 wavamia na kujeruhi wanakijiji

Na SAMUEL BAYA

MWAKA mpya ulianza kwa mkosi katika kijiji cha Kagujo, Mishomoroni kaunti ya Mombasa baada ya genge la majambazi sita kuvamia kijiji hicho na kuwashambulia wakazi.

Genge hilo lililokuwa na mapanga na mijeledi lilivamia kijiji hicho saa sita unusu wakazi walipokuwa wakisherehekea mwaka mpya.

Watu watano walipata majeraha ya kichwa na mikono baada ya kukatwa pamoja na kupigwa na vifaa butu.

Shambulizi hilo ambalo wakazi wanadai lilidumu kwa takribani dakika kumi lilitekelezwa na vijana ambao walikuwa wamejiziba usoni na kubeba rungu, mapanga na visu.

Mmoja wa wakazi kwa sasa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja eneo la Kisauni. Wengine walitibiwa na kurushuwia kurudi nyumbani.

Mmoja wa waathiriwa hao Bi Kahaso Kaingu aliambia Taifa Leo nyumbani kwake kwamba, walikuwa wameanza kufurahia kwa shangwe za mwaka mpya vijana hao walipotokea na kuwavamia.

“Tulikuwa tunaendelea kusherehekea mwaka mpya wakati nilimuona mmoja wa majirani akitoroka mbio. Niliposimama kuangalia kilichokuwa kikjjiri, mara vijana hao walitokea wakiwa na visu na mapanga. Hapo ndipo mmoja aliponikata kichwani kisha akanipiga tena kwa kifaa butu. Nilianguka nikibubujikwa na damu,” akasema Bi Kaingu.

Baadaye, alisema, wasamaria wema walimpeleka kwa pikipiki hadi katika hospitali moja eneo la hilo Kisauni.

“Kwa kweli hali ni mbaya sana katika eneo hili. Ninaomba tu serikali iingilie kati na kukabiliana na utovu wa usalama katika sehemu hii,” akasema Bi Kaingu, huku akionyesha jeraha kubwa la kichwa.

Muathiriwa mwingine Bw David Lewa ambaye ni mwalimu katika shule moja jirani aliambia Taifa Leo kwamba, alikuwa amefika katika eneo la tukio kuukaribisha mwaka kwa kujivinjari alipovamiwa na kukatwa kichwa. “Ninasikia uchungu. Wamenipiga kichwa na kuniumiza,” akasema mwalimu huyo huku akiwa na maumivu makali ya kichwa. Wakazi walidai polisi hutembelea mahali hapo na kuondoka mapema.

  • Tags

You can share this post!

Mbwembwe za Mwaka Mpya 2019

Wakenya waliteseka 2018, watarajia hali bora 2019

adminleo