Mwanablogu aliyeshtakiwa kuandika taarifa za kupotosha kuhusu Gavana aachiliwa
MWANABLOGU aliyeshtakiwa kuchapisha taarifa za kupotosha kuwa Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro aliibiwa Sh200 milioni amekuwa huru baada ya kupunguziwa dhamana.
Bw Jimmy Charles Mureithi alililia Hakimu Mkuu Mkazi David Odhiambo kuwa dhamana ya Sh500,000 aliyopewa awali ilikuwa ghali mno na kuomba ipunguzwe ili apate kuondoka korokoroni huku akisubiri kesi yake kuendelea.
Bw Odhiambo alipunguza dhamana hiyo kutoka Sh500,000 hadi Sh100, 000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.
Bw Mureithi alijipata pabaya baada ya kudaiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wa kijamii ya Facebook akidai kuwa mfanyabiashara Loise Makena alimuibia Bw Mun’ngaro fedha hizo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa madai hayo yalimharibia sifa mfanyabiashara huyo.
Jamaa huyo alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo kinyume na Kifungu cha 23 cha Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Makosa ya Mtandao ya mwaka 2018.
Karatasi ya mashtaka inaonyesha kuwa Bw Mureithi alichapisha habari kwenye mitandao ya kijamii kwamba Bi Makena alimlaghai Bw Mun’garo pesa hizo.
Upande wa mashtaka unasema kuwa taarifa hizo zilidhalilisha sifa ya mfanyabiashara huyo.
Mahakama ilifahamishwa kuwa mshukiwa alisambaza habari hizo za uzushi kwenye mtandao wa kijamii akitumia jina la akaunti ya Facebook ‘Mureithi Wa Lucy.’
Inadaiwa kuwa mshukiwa huyo alitenda kosa hilo katika eneo na muda usiojulikana.
Mshukiwa huyo hata hivyo alikanusha shtaka hilo alipofika mbele ya Hakimu Odhiambo juma lililopita.