Habari Mseto

Mwanablogu Maverick Aoko ashtakiwa kuchapisha habari za kusumbua na kuudhi

Na RICHARD MUNGUTI August 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANABLOGU Scophine Aoko Otieno almaarufu Maverick Aoko Otieno ameshtakiwa kwa kuchapisha habari za uwongo katika mitandao ya kijamii.

Aoko aliyetiwa nguvuni Ijumaa mnamo Agosti 16, 2024 alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Susan Shitubi Jumatatu mnamo Agosti 18, 2024.

Alikanusha mashtaka matatu yaliyomkabili ya kuchapisha habari za uwongo, kusumbua katika mtandao na kutumia mtandao wa kijamii kwa njia isiyofaa.

Aoko alikana mashtaka dhidi yake kisha akaomba aachiliwe kwa dhamana.

Mashtaka dhidi ya Aoko yalisema alichapisha habari za uwongo, kumshushia mlalamishi hadhi yake.

Hakimu alifahamishwa mshtakiwa alimharibia jina mmoja “Amber Ray na Jamal” na kumharibia taaluma Beth Wambui Mbuitu.

Kiongozi wa mashtaka Wanjiru Waweru alieleza korti kwamba mshtakiwa alichapisha “habari hizo akijua zililenga kumshushia hadhi mlalalamishi kwa kuchapisha habari za uwongo na za kupotosha.”

Pia mahakama ilifahamishwa habari hizo zilikuwa zinalenga kumsababishia woga mlalamishi.

“Habari hizi zililenga kumharibia sifa na taaluma Beth Wambui Mbuitu,” Bi Waweru alielezea korti huku akipinga polisi wasimrudishie simu ya rununu na laptop zilizotwaliwa na polisi walipomtia nguvi mshtakiwa.

Aoko alikanusha kwamba alichapisha habari hizo za kuudhi mnamo Agosti 3, 2024.

Wakili Ateka Ingati anayemwakilisha mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana akisema “itakuwa habari njema kwa wanablogu wenzake kwamba korti imetilia maanani maslaha ya jamii nzima ya wanablogu.”

Wakili huyo alishangaza korti aliposema polisi wamemshtaki Aoko na makosa ambayo hawakuchunguza.

“Polisi walipewa idhini na mahakama kuchunguza madai 21 ya uhalifu wa kimitandao dhidi ya mshtakiwa lakini sasa wamewasilisha shtaka tofauti,” alisema Bw Ingati.

“Mheshimiwa, polisi walikuwa wanachunguza mawasilisho 21 katika mitandao ya kijamii dhidi ya Aoko. Lakini sasa wameshtaki kwa mambo mengine tofauti,” Bi Ingati aliambia korti.

Wakili huyo aliomba korti ishurutishe polisi kumrudishia Aoko simu na laptop akisema hazihitajiki katika kesi hii inayomkabili mshtakiwa.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bi Wanjiru Waweru alipinga ombi la kumrudishia Aoko vifaa vilivyotwaliwa na polisi.

Akitoa uamuzi iwapo Aoko ataachiliwa kwa dhamana, Bi Shitubi aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh100,000 hadi Septemba 2, 2024 kesi itakapoanza kusikizwa.

Na wakati huo huo hakimu alikataa kuamuru polisi wamrudishie simu na laptop mshtakiwa akisema “ni ushahidi.”

Hakimu alisema polisi wakikamilisha kuchunguza simu na laptop hiyo, mshtakiwa anaweza kuomba arudishiwe.

Bi Shitubi alielezwa vifaa hivyo ndivyo Aoko anatumia kufanyia kazi.