Habari Mseto

Mwanafunzi apatikana amefariki katika chuo kikuu cha Moi

November 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

MWANAFUNZI wa kiume wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret amepatikana amefariki chumbani mwake katika bweni la wanafunzi katika eneo la Kesses katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Marehemu ambaye anasomea shahada ya elimu aMEpatikana amelala kitandani akiwa amefariki.

Marafiki wake ambao walikuwa wamemtembelea chumbani mwake wamekumbani na maiti yake kitandani mwake.

“Tumepata mwenzetu akiwa amefariki kitandani mwake. Hatujajua chanzo cha kifo chake,” amesema mmoja wa marafiki wa mwendazake.

Kifo hicho kimeongezea wasiwasi wa wanafunzi kuhusu usalama wao chuoni humo.

Baadhi ya wanafunzi ambao hawakutaka kutajwa wamesema kuwa hali ya usalama wa wanafunzi katika eneo hilo inaendelea kuwa tete kila uchao.

Kando ya mwili wa marehemu kulikuwa na dawa ambapo haijabainika iwapo marehemu alikuwa akiugua.

Akithibitisha kisa hicho kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Kesses Aaron Muriasi amesema kwamba huenda mwanafunzi huyo alikuwa mgonjwa maradhi ambayo bado hayajatambuliwa baada ya madawa kupatikana chumbani mwake.

Maiti ya marehemu aliyekuwa na umri wa miaka 22 imepelekwa katika mochwari ya hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret

“Ni mapema kubaini chanzo cha kifo hiki. Tumepeleka mwili katika chumba cha maiti MTRH ambapo upasuaji wa maiti utabaini chanzo cha kifo hicho,” amesema Bw Muriasi.

Afisa huyo ameongeza kuwa polisi wameanzisha uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho.