Habari Mseto

Mwanahabari wa NMG ateuliwa kijana bora wa mwaka

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MWANAHABARI wa masuala ya teknolojia katika kampuni ya Nation Media Group (NMG), Faustine Ngila ameteuliwa kama Kijana Bora wa Mwaka katika kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) kwenye Tuzo za Top 35 Under 35 mwaka 2020.

Tuzo hizo zinazoandaliwa na shirika la Youth Agenda kwa ushirikiano na Wizara ya Teknohama na Masuala ya Vijana nchini Kenya, zilivutia zaidi ya vijana 3,000 ambapo kupitia mchujo, 135 waliteuliwa kuunga orodha ya mwisho.

Bw Ngila ambaye amejizolea sifa nchini kwa kuripoti kuhusu masuala ya teknolojia za kisasa, aliashiria furaha yake kwa uteuzi huo wa kipekee.

“Ninashukuru NMG kwa kunipa nafasi na majukwaa mwafaka ya kuangazia masuala ya teknolojia. Nina furaha kuteuliwa na Youth Agenda ambao wamenipa fursa ya kukuza na kuwasaidia vijana wenzagu,” alisema mwanahabari huyo anayeandikia magazeti ya Taifa Leo, Daily Nation, Business Daily, The EastAfrican na Daily Monitor yanayomilikiwa na NMG.

Hafla ya kuwatuza vijana hao 135 katika vitengo 15 tofauti vya mwaka huu, itafanyika Agosti 12 ikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta atakayewaongoza Wakenya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana.

“Tulitafuta wawaniaji wa vitengo vyote 15 kati ya Mei na Juni 2020 na jopo la waamuzi 24 likatoa orodha ya wawaniaji 135 waliounga orodha fupi. Sasa tunapania kupata washindi wawili wa mwisho (mmoja wa kike na mmoja wa kiume) katika kila kitengo,” akatanguliza Afisa wa Mawasiliano wa Youth Agenda, Muthengi Mbuvi.

“Tutawatambua na kutuza washindi wote mnamo Agosti 12 na baadaye kuwapa mafunzo ya masuala ya uongozi kwa ushirikiano na taasisi na mashirika mengine kwa kipindi cha mwaka mmoja,” akaongeza Mbuvi.