Habari Mseto

Mwanamasumbwi wa Nigeria alalamika kutupwa kwa seli chafu Kenya

February 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MWANADONDI kutoka Nigeria alimshangaza hakimu mkuu mahakama ya milimani Nairobi Francis Andayi alipomweleza seli za korti ni chafu na vyoo vinatoa uvundo, Ijumaa.

Na wakati huo huo Bw Sije Brown Chidinma aliwakashfu maafisa wa usalama wa Kenya na maafisa wa uhamiaji kwa kumtesa walipokuwa wanamtia nguvuni.

“Taaluma yangu ni uanamasumbwi lakini nimeshangaa jinsi maafisa wa idara ya uhamiaji na polisi walivyonichukua kama mimi sio mtu kutoka barani Afrika.”

Akaongeza Bw Chidinma, “Naomba kuelezea masikitiko yangu kwa kuchukuliwa ni kana kwamba natoka bara lingine. Nchi hii ya Kenya iko barani Afrika na sijapendezewa na jinsi nilitendewa na kuchukuliwa. Tulikamatwa tukiwa na Mzungu na kuzuiliwa ndani ya seli lakini leo nimefika kortini nikiwa peke yangu. Mzungu huyo yuko wapi na alikuwa ametiwa nguvuni kwa kupatikana na pasi mbili za kusafiria?” akachemka Bw Chidinma.

Mshtakiwa huyo alikanusha shtaka la kupatikana ameghushi pasi yake ya kusafiria katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta akielekea Oslo nchini Norway.

Akijibiwa na hakimu kuhusu usafi wa seli , alimweleza sheria imetolewa kuhakikisha usafi umedumishwa katika magereza.

“Nimeenda nchi nyingi na usafi upo. Mbona choo za hapa kortini zanuka?” aliuliza Bw Chidinma.

Bw Andayi alimweleza kuwa kuna mwongozo mahakama ziwe zikitembelea idara ya magereza kuhakikisha mazingira ni safi.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 ama alipe pesa taslimu Sh300,000.

Kesi inayomkabili itasikizwa Machi 12, 2019.