Habari Mseto

Mwanamke adai mpenziwe mwanajeshi alimteka nyara na kumpiga

May 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TITUS OMINDE NA LABAAN SHABAAN

POLISI mjini Eldoret wanachunguza madai ya mfanyakazi wa Idara ya Mahakama anayesema alitekwa nyara na kudhulumiwa na mpenzi wake.

Bi Violet Indiasi anadai kuwa mchumba wake ‘mfanyakazi katika Idara ya Ulinzi (KDF)’ alimwalika jijini Nairobi mnamo Januari 15 kabla ya kumteka nyara na kumnyanyasa kinyama.

Kwa mujibu wa mlalamishi, alielekezwa kukutana na mpenzi wake Murang’a kabla ya kupelekwa katika msitu wa Maragwa.

Mshukiwa anadaiwa kuiba pesa zilizohifadhiwa katika rununu ya Bi Indiasi kwa kutuma kwenda kwenye namba nyingine ya simu.

“Nilipitia taabu nyingi sana usiku huo na kuachwa msituni. Nilijikokota hadi kijiji kilichokuwa karibu ambapo nilisaidiwa na mzee fulani kuripoti kisa hicho kwa polisi,” alieleza.

Alipiga ripoti katika vituo viwili vya polisi vya Kapsoya na Eldoret Central vilivyonakili maelezo ya matukio ya usiku wa Januari 14 na 15.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Uasin Gishu Benjamin Mwanthi amethibitisha haya na kusema uchunguzi unaendelea.

Lakini Bi Indiasi analaumu vyombo vya usalama akilalamai wamechukua muda mrefu kukamilisha uchunguzi.

“Nina miezi minne sasa nikiwa na kiwewe lakini polisi wanachukulia suala langu hivi hivi tu,” aliteta.

Bw Mwanthi amefafanua kuwa kisa hiki ni maalum kwa sababu kinahusisha afisa wa jeshi.

Anadokezi kuwa baada ya kukamilisha upelelezi, faili itatumwa kwa KDF ili wachukue hatua kwa mujibu wa utaratibu wao.

Kupitia wakili wake Evans Miyienda, Bi Indiasi amefichua kuwa wanajuana na mshukiwa na wote ni wakazi wa kaunti ya Vihiga.

Kadhalika, mshukiwa anadaiwa kudukua akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook.

“Ninashangaa kwa nini ni ngumu kwa polisi kumkamata licha ya kupewa maelezo yote yakiwemo majina yake na anakofanyia kazi. Maisha yangu yako hatarini.,” alilia Bi Indiasi.

Mshukiwa anadaiwa kufanya kazi katika kambi ya jeshi ya Moi Airbase jijini Nairobi.

Wakili Miyienda anaarifu kuwa alifuata suala hilo hadi katika makao makuu ya Idara ya Ulinzi lakini juhudi zake zimegonga mwamba.

Aliahidiwa kuwa hatua za kisheria zingechukuliwa iwapo mshukiwa angepatikana kuwa mfanyakazi wa KDF.