Mwanamke ajeruhiwa katika mkasa wa moto Elburgon
NA JOHN NJOROGE
MWANAMKE mwenye umri wa miaka 30 amepata majeraha mabaya Alhamisi asubuhi baada ya nyumba yake kushika moto katika mtaa wa Salama mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru.
Akithibitisha kisa hicho, naibu chifu wa eneo hilo Bw Steve Mwangi alisema chanzo cha moto huo ulioanza mwendo wa saa tatu asubuhi hakikubainika mara moja.
Lakini Bw Mwangi alisema kuwa mali ya thamani iliteketea.
Bi Anne Wangui, ambaye ni jirani ya mwathiriwa, alisema alikuwa ndani ya nyumba yake aliposikia majirani wakilia na kupiga mayowe.
Alipotoka nje, alisikia mwanamke, ambaye nyumba yake ilikuwa ikiteketea, akiomba msaada.
Mwanamke huyo pia alikuwa na majeraha ya moto.
“Nyumba yake ilikuwa bado inawaka moto. Kwa kuwa sikuwa najisikia vizuri, nilipoteza fahamu kufuatia tukio hilo. Lakini majirani wengine walimiminika eneo la tukio kuzima moto kabla ya lori la zimamoto kutoka kaunti ndogo ya Molo kufika na kuuzima kabisa,” akasema Bi Wangui.
Mbali na nyumba hiyo ya mwanamke aliyepata majeraha, pia nyumba za familia nyingine mbili ziliteketea.
Bi Wangui alitoa wito kwa serikali na viongozi wa eneo hilo kusaidia familia zilizoathiriwa.
Ilisadifu kwamba Taifa Leo ilimhoji mkazi mwingine mwenye jina linalofanana na la Bi Wangui.
Mkazi huyo mwingine, Bi Anne Wangui, aliyekuwa akipita karibu na eneo hilo la moto, alisema alimkuta mwanamke huyo akihema kwa maumivu huku akiomba kusaidiwa kupelekwa hospitalini.
“Baada ya kumpeleka katika zahanati iliyo karibu, tulimhamisha hadi hospitali ya Kaunti Ndogo ya Elburgon kwa matibabu kwani majeraha aliyopata yalikuwa makubwa,” alisema bI Wangui na kuongeza kuwa mwanamke huyo alilazwa katika kituo hicho, matibabu yakianza upesi.
Alisema mwanamke huyo alipata majeraha ya moto usoni, kichwani na miguuni.
Alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa matukio kama hayo yanazuiwa kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya moto kama vile mishumaa, mitungi ya gesi miongoni mwa vingine viko katika sehemu salama isiyoweza kufikiwa na watoto.
Mkasa huo umetokea miezi michache tu baada ya mvulana wa umri wa miaka miwili na nusu kufa katika tukio la moto katika nyumba yao, mita chache kutoka eneo la tukio la Alhamisi.