Habari Mseto

Mwanamke aliyehusika katika mauaji ya mwanamume Mholanzi aomba ahurumiwe

June 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

MWANAMKE aliyeshtakiwa kwa kuhusika katika mauaji ya raia wa Uholanzi Herman Rouwenhorst, ameomba mahakama imuhurumie kwani anajuta kuhusika katika uhalifi huo.

Bi Mary Ambani Nekesa, ambaye alikiri kuhusika katika kupanga mauaji hayo, alimwambia Jaji Ann Ong’injo kuwa anajutia kitendo chake na kuomba ahurumiwe ili aweze kuwatunza watoto wake.

“Ninajuta kwa kuhusika katika tendo hilo, nimejifunza kutokana na makosa yangu. Ninaomba mahakama hii inionee huruma kwa kunipa hukumu yenye adhabu ya chini,” alisema kupitia kwa wakili wake.

Aliambia mahakama kwamba yeye ni mama wa watoto wawili na angetamani apewe adhabu ya chini ambayo itamruhusu kuwatunza watoto hao.

Mshukiwa huyo ambaye aligeuzwa kuwa shahidi wa upande wa mashtaka, alisema alitengana na baba wa watoto hao wakati wa tukio hilo la 2021, na kuachwa na jukumu la kuwalea watoto hao peke yake.

Alidai kuwa, tangu aachane na mumewe, jamaa huyo hajawahi kushughulikia watoto hao kwa njia yoyote.

“Watoto wangu wamekuwa wakikaa na shangazi yao ambaye pia ni mjane tangu nilipokamatwa mwaka wa 2021. Naiomba mahakama inihurumie kwa ajili ya watoto wangu,” alisema.

Mwanamke huyo pia alisema amejifunza ujuzi muhimu katika muda wa miaka mitatu ambao amekuwa gerezani ambao utamsaidia kukabiliana na maisha nje ya kuta za gereza.

Bi Nekesa alishtakiwa pamoja na mjane wa Bw Rouwenhorst, Riziki Ali Cherono na Timothy Omondi Ngowe almaarufu kama Tony Ochieng’ akifahamika pia kama Mohamed Khalid, kwa mauaji ya Mholanzi huyo pamoja na mlinzi Evans Pole Bokoro.

Wanadaiwa kutekeleza hayo mnamo Juni 4, 2021.

Hata hivyo, Bi Nekesa aliingia katika maafikiano ya makubaliano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na sasa ni shahidi wa upande wa mashtaka.

Kutokana na makubaliano haya, serikali ilimpunguzia mashtaka, na kumshtaki kwa mauaji bila kukusudia badala ya mauaji.

Bi Nekesa amekiri makosa mawili ya kuua bila kukusudia. Mahakama iliambiwa kwamba mshukiwa huyo aliwaua Rouwenhorst na Bokoro kinyume cha sheria.

Kulingana na rekodi za mahakama, Bi Nekesa alitumiwa kuwezesha wahalifu kuingia katika Roco Apartments kwa Bw Rouwenhorst, mtaani Shanzu usiku wa manane.

Rekodi ya mahakama inaonyesha usiku wa Juni 3, Bi Nekesa aliingizwa kwenye chumba kisichokuwa na mtu ndani ya jumba hilo.

Inadaiwa kuwa mshukiwa huyo alimsaidia Bw Omondi kuingia katika boma la marehemu kabla ya kutekeleza mauaji hayo usiku wa manane.

“Mshukiwa alimuambia Bw Bokoro kuwa Bw Omondi alikuwa mgeni wake. Hili lilihakikisha kuwa jamaa huyo aliingia katika boma hilo bila kushukiwa kuwa alikuwa na nia mbaya,” alisema kiongozi wa Mashtaka, Bw Benard Ngiri.

Rekodi za mahakama zinaonyesha zaidi kuwa Bi Nekesa alimtambulisha Bi Cherono kwa Bw Omondi kabla ya kisa hicho.

Bi Cherono alidaiwa kumweleza rafiki yake Nekesa kuhusu nia yake ya kumuua mumewe, Rouwenhorst.

Bw Omondi ndiye aliyechaguliwa kutekeleza mauaji hayo. Bi Nekesa anasubiri kuhukumiwa.