Mwanamke aliyejeruhi wanawe kwa kisu afungwa kifungo cha chini ya uangalizi kwa miaka mitatu
Na BRENDA AWUOR
MWANAMKE mwenye umri wa miaka 29 aliyewajeruhi wanawe wanne kwa kuwadunga kisu cha nyumbani kisha kujidunga shingoni eneo la Awasi, atafungwa kifungu cha chini ya uangalizi na cha lazima kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mercy Anyang’o aliyeshtakiwa kosa la kujaribu kuua wanawe wanne kwa kuwadunga shingoni na tumboni kwa kisu cha nyumbani mnamo Januari 7, 2020, eneo la Awasi, alipewa hukumu ya kifungo na Hakimu mkazi mkuu Reuben Sang wa mahakama ya Nyando.
Anyang’o alikiri makosa ya kujaribu kuua watoto wake – wavulana wawili na msichana mmoja na kisha kujidunga kwa kisu hicho.
Atafungwa kifungu cha chini ya uangalizi na cha lazima kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kuomba korti imwachilie huru ili alinde wanawe.
Hakimu Sang aliamuru Anyang’o afungwe kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya mshtakiwa kujieleza na kuomba korti kumwacha huru.
Alijitetea kuwa kilichotokea kilikuwa ni hasira kutokana na hali kwamba mumewe aliwatoroka nyumbani.
“Kutokana na ushahidi tulio nawe ni wazi kuwa ulikuwa na lengo la kuua wanao wanne kisha nawe ujiue; hivyo basi utafungwa kifungu cha miaka mitatu chini ya uangalizi,’’ hakimu aliamuru.
Mnamo Februari ripoti kutoka hospitali ya rufaa na mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) ilionyesha kuwa mwanamke huyo alikuwa na akili timamu anayestahili kupokezwa hukumu yoyote kulingana na vitendo vyake.
Anyang’o alifanyiwa ukaguzi na uchunguzi wa kiakili baada ya kiongozi wa mashtaka Bi Maureen Odumba, kuomba korti ya Nyando, iruhusu uchunguzi wa kiakili kufanywa kabla ya hukumu kutolewa mnamo Januari 24, 2020, kesi ilipokuwa ikisikilizwa.
Mshtakiwa alieleza kuwa mumewe Bw Maurice Ochieng, alikuwa amepata mchumba mwingine na kumtoroka pamoja na wanawe wanne; kitendo kilichompa hasira na kusababisha atekelezo kitendo cha kuwadunga wanawe kisu.
“Naomba korti inisamehe. Ilikuwa ni hasira kwa sababu ya vitendo vya mume. Bado nawapenda wanangu na nitawashughulikia,’’ Bi Anyang’o aliomba.
Waathirika wote ambao walipelekwa katika hospitali ya JOOTRH na majirani ili kupokea matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata, wamepelekwa katika eneo la kuchunga watoto Achego, Kisumu.