• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Mwanamke aliyekuwa na seneta hotelini kuzuiliwa seli kwa siku saba

Mwanamke aliyekuwa na seneta hotelini kuzuiliwa seli kwa siku saba

Na RICHARD MUNGUTI

MWALIMU wa shule ya sekondari aliyekuwa na Seneta wa Machakos, Boniface Mutinda Kabaka usiku aliozirai ndani ya hoteli moja jijini Nairobi, huenda akafunguliwa shtaka la kujaribu kumuua mwanasiasa huyo.

Polisi walimwambia Hakimu Mwandamizi Daniel Ndungi kwamba Bw Kabaka angali hali mahututi hospitalini na hivyo wanahitaji muda zaidi kumzuilia Bi Esther Nthenya Muli, 45.

Afisa anayechunguza kisa hicho, Konstebo Jason Matete, alisema mashtaka yatategemea hali ya seneta huyo itakavyokuwa.

Akiwasilisha ombi la mwalimu huyo azuiliwe kwa siku saba, Bw Matete alisema wawili hao walikuwa wanakula na kunywa katika hoteli moja ambapo Bw Kabaka alikuwa amekodisha chumba nambari 306, Desemba 3, 2020.

Mchunguzi huyo alieleza korti kuwa wawili hao walipelekewa chakula na vinywaji ndani ya chumba chao na wafanyakazi wa hoteli hiyo.

Korti iliambiwa kuwa mwendo wa saa saba za usiku, wafanyakazi wa hoteli walielezwa na Bi Muli kuwa Bw Kabaka ameugua na ambulensi kutoka Nairobi Hospital iliitwa na kumpeleka Bw Kabaka hospitali.

“Bw Kabaka aliingia katika hoteli mnamo Desemba 3. Alionekana buheri wa afya. Mwendo wa saa saba kasoro dakika 14, Desemba 4, 2020 seneta alianza kutapika kisha akaanguka na kuzirai,” hakimu alifahamishwa.

DHAMANA

Wakili wa mshukiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema Bi Muli ni mwalimu na hawezi kutoroka ama kuvuruga ushahidi kama ilivyodaiwa na Bw Matete.

Akitoa uamuzi, Bw Ndungi aliamuru Bi Muli azuiliwe hadi hali ya Bw Kabaka, ambaye amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi itakapojulikana.

Bw Ndungi aliombwa na Bw Matete aamuru mshukiwa huyo asalie rumande ahojiwe na kusaidia wachunguzi kukamilisha mahojiano.

Mahakama ilisema polisi wanahitaji muda kuchunguza sampuli za vyakula na vinywaji ambavyo wawili hao walikuwa wanatumia kabla ya Bw Kabaka kuanza kutapika na hatimaye kuzirai.

Sampuli hizo zimepelekwa katika maabara ya Serikali kupimwa ili kubaini iwapo mwanasiasa huyo aliwekewa sumu.

Kesi itatajwa Jumanne ijayo.

You can share this post!

Uhuru aenjoi vijana

SHINA LA UHAI: Mzigo wa HIV na Kansa ya mlango wa uzazi kwa...