• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Mwanamke aliyetoweka miaka 24 arudi kwao na watoto 7

Mwanamke aliyetoweka miaka 24 arudi kwao na watoto 7

Na BRIAN OJAMAA

FAMILIA moja katika kijiji cha Misimo, eneobunge la Webuye Mashariki, Kaunti ya Bungoma ilipigwa na butwaa baada ya binti yao aliyepotea miaka 24 iliyopita kurejea nyumbani akiwa na watoto saba.

Kulingana na Wafula Wasilwa ambaye ni jamaa ya Agnes Nelima, familia yao ilikuwa imepoteza matumaini kwani walidhani alikuwa ameaga dunia kitambo.

“Tulimtafuta kila mahali na hata tukapiga ripoti polisi na katika vyombo vya habari lakini hatukuweza kumpata. Wazazi wetu walimtafuta na walifariki kabla hawajampata. Tumefurahi amerejea nyumbani na pia tunajua wazazi wetu wana furaha walipo,” akasema nduguye.

Mwanamke huyo alikaribishwa na familia yake kwa vifijo na nderemo kwenye sherehe iliyohudhuriwa na majirani wengi.

“Tumemwandalia chakula maalum cha kumkaribisha. Pamoja na majirani tunasherehekea kurudi kwake. Tunamshukuru Mungu kwa kuwa mwenzetu amerudi nyumbani akiwa buheri wa afya kwani tulidhani alikuwa amefariki. Kupotea kwa miaka 24 si mchezo,” akasema nduguye.

Mwanamke huyo alitoweka mnamo 1996 alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha pili.

Akisimulia kisa chake, mwanamke huyo alisema kuwa alitoroka na kijana ambaye alimuoa na wakahamia Uganda ambako wanaishi pamoja hadi leo.

“Nasikitika wazazi wangu walifariki baada ya kunitafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. Naona makaburi yao lakini naomba msamaha kwao na jamaa zangu pia. Niliogopa kuja nyumbani kwani nilihofia ningeadhibiwa vikali kwa kukosa kukamilisha masomo ya sekondari,” akasema Bi Nelima na akawapongeza jamaa zake kwa kumpokea kwa moyo mkunjufu.

“Nafurahi kufika nyumbani. Pia, nawashukuru jamaa zangu kwa kunikubali tena. Wamenipa mwaliko mzuri na nimefurahi. Mungu ni mwema kwa kuniwezesha kujumuika nao tena,” akasema.

Richard Wafula ambaye ni mzee wa kijiji alisema kuwa hakuna matambiko yeyote yatafanyika, licha ya Bi Nelima kurejea nyumbani baada ya miongo miwili.

“Yeye ni mwanamke. Kama angekuwa mwanaume tungemfanyia matambiko kabla akubaliwe tena katika jamii,” Bw Wafula alisema.

  • Tags

You can share this post!

Nilikuonya, Mutula Junior amkumbusha Ole Kina

Sonko amkabidhi Uhuru usimamizi wa Nairobi

adminleo