Habari Mseto

Mwanamke anayeshtakiwa kumuua mpenziwe azuiliwa

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Richard Munguti

Mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ameagizwa azuiliwe hadi Mei 2 kuhojiwa kwa mauaji ya mpenziwe.

Zeitun Abdul aliyekuwa amempakata mtoto mchanga aliagizwa azuiliwe kwa siku 17.

Kiongozi wa mashtaka Patience Mbange aliambia mahakama mshukiwa huyo anadaiwa kumuua mpenziwe.

“Kwa mujibu wa uchunguzi marehemu na Zeitun walitofautiana Aprili 15 huku wakilaumiana kwa kuwa na mipango ya kando,” Bi Mbange alieleza hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Muthoni Nzibe.

Mahakama ilifahamishwa wapenzi hao waliteta hadi mate yakageuka pofu kabla ya ” Zeitun kujihami kwa kisu na kumfuma mpenziwe kifuani upande wa kushoto.”

Maskini mpenziwe Zeitun alipiga kamsa kwamba ” umeniua.”

Kiongozi huyo wa mashtaka alisimulia kwamba mayowe na sauti ya uchungu ya mhasiriwa yaliwavutia majirani.

Majirani wema walifika kutoa msaada wa dharura kufuatia wito wa mwendazake asaidiwe.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Sajini Vincent Batinya amedokeza katika taarifa ya kiapo kwamba mhasiriwa alipelekwa hospitali ya Mbagathi alikotangazwa “ameaga alfajiri ya Aprili 16 2020 alipopelekwa kupata huduma ya kwanza.”

Hakimu aliombwa aamuru mshukiwa azuiliwe kwa siku 17 ahojiwe na mashahidi wengine kuandikisha taarifa zao.

Hakimu alielezwa upasuaji kubaini kilichopelekea mhasiriwa kuaga haujafanywa pamoja na kutayarisha picha za mahala pa tukio hilo.

Mahakama iliambiwa kisu alichokitumia kumtoa uhai mwendazake kilipatikana nyumbani kwao eneo la Lindi , Kibra Nairobi.

Mahakama pia ilielezwa uchunguzi wa DNA haujakamilishwa pamoja na ripoti ya utimamu wa akili wa Zeituni kutolewa na mtaalam wa tiba za ubongo.

Akiruhusu ombi la Sajini Batinya Bi Nzibe alisema mshukiwa huyo anadaiwa ametenda kosa mbaya ambayo akipatikana na hatia huenda “akapata kifungo cha maisha ama kuhukumiwa kunyongwa.”

Bi Nzibe alisema polisi wanahitaji kupewa muda kukamilisha uchubguzi.

Aliwapa polisi muda wa siku 17 kukamilisha uchunguzi huo.

“Utazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani kuhojiwa kuhusu mauaji ya mpenzio kwa siku 17,” hakimu aliamuru.