• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Mwanamke aokolewa baada ya kushambuliwa na mumewe kwa kukosa kuandaa mlo

Mwanamke aokolewa baada ya kushambuliwa na mumewe kwa kukosa kuandaa mlo

Na SAMMY KIMATU

MWANAMKE wa umri wa miaka 26 aliokolewa na maafisa wa kushughulikia kesi za Dhulma za Kijinsia (GBV) Jumatatu baada ya tukio la kusikitisha ambapo alishambuliwa na mumewe.

Sababu ya kupiga inadaiwa ni kwa kukosa kupika chakula cha jioni.

Tukio hilo lilitokea katika eneo la Crescent katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba katika wadi ya Land Mawe iliyoko kaunti ndogo ya Starehe.

Mwathiriwa, Bi Jackline Kageni, mama mzazi wa watoto watatu, alipigwa na mume baada ya kukosa kununua chakula cha jioni.

Aidha, alisema alitoka Kaunti ya Meru kabla ya kuolewa na mumewe Bw Gipson Kayu, mwenye umri wa miaka 38 kutoka Kaunti ya Kisii. Kulingana na Jackline, shida ilianza wakati mume alimpa Sh100 kununua chakula cha jioni.

Alisisitiza kuwa pesa hazitoshi kununua chakula kwa familia ya watu watano na kuongeza kuwa mume alikuwa na pesa zaidi lakini badala yake alienda kununua viatu vyake badala ya kupeana pesa za chakula.

Mwathiriwa, Bi Jackline Kageni, mama mzazi wa watoto watatu, alipigwa na mumewe eneo la Crescent, Nairobi. Picha/ Sammy Kimatu

Fauka ya hayo, alisema kuwa mume ni mraibu wa dawa za kulevya ambaye alikuja nyumbani akiwa amelewa chakari.

Kwa upande wake, Bw Kayu aliambia Taifa Leo kwamba alikuwa amechoka baada ya kuchapa kazi ngumu siku hiyo kutoka kwa kampuni moja ya kutengeneza unga wa ugali na wa ngano katika eneo la Viwanda ambapo ameajiriwa kama kibarua wa kupakia magunia ya nafaka.

“Nilitoka nyumbani muda mfupi baada ya mke wangu kuondoka saa kumi na mbili na nusu asubuhi bila hata kuandaliwa kiamsha kinywa. Kazini, ambapo nilipakua magunia ya mahindi sikula chakula cha mchana pia. Wakati wa jioni, nilitaka kula ‘chakula kizito cha jioni’. Badala ya anunue chakula, mke wangu alitumia pesa hizo kulipa deni la nguo yake aliyokuwa amenunua. Nilitarajia kwa pesa ambazo nilikuwa nimempa atanunua mayai, ’’ Bw Kayu aliongeza.

Kitendo hicho kilimkasirisha mume huyo na ndipo ubishi mkali ulizuka na vita ya mke na mumea ikaanza.

Bw Kayu alidai hasira zilimpanda zaidi baada ya mkewe kumshambulia akitumia sufuria. Maji yalipozidi unga, wanawake majirani katika mtaa huo walitoka kwa wingi kuja kumnusuru mwanamke huyo baada ya kupiga kamsa akitaka asaidiwe. Mume alikutana na ghadhabu ya wanawake hao ambao walimkabili na kumchapa kumchapa kichapo cha mbwa msikitini.

Bw Kayo alilalamika alikuwa na maumivu ya kichwa, mbavu na miguu kufuatia kichapo alichopata.

Afisa wa Masuala ya Dhulma za Kijinsia katika mtaa wa Mukuru, Bi Jane Mbula Kyalo alisema familia hiyo ilikuwa na mizozo kadhaa hapo awali na ilikuwa ni mizozo ambayo haijawahi kumalizika.

Vile vile, aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa mwanamume huyo pindi mwanamke atakapopata Fomu ya P3 kutoka kwa polisi.

Akiongea na wanahabari kuhusu tukio hilo,  Msaidizi wa Kamishna wa Kaunti wa South B, Bw Michael Aswani Were alikashifu tukio hilo na kushauri jamii ya Mukuru isuluhishe mizozo ya kifamilia kupitia Kamati ya Nyumba Kumi, wenyeviti na wazee wa mitaa, machifu na manaibu wao pamoja na viongozi wa dini.

Kadhalika, Bw Were alifafanua kuwa vita, mizozo ya famila na waume kuwajeruhi na kuwaumiza wake zao ni kosa kubwa inayostahili adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

“Tafuta njia za upatanisho kupitia viongozi wa dini, majirani, maafisa wa Nyumba Kumi na wasimamizi. Usichukue sheria mikononi mwako kwa sababu tutakuja kwako kukutia baroni kwa kukiuka sheria za nchi, ” Bw Were asema. Kadhalika, alisisitiza tena kuwa mshukiwa atakamatwa na kushtakiwa kortini mara tu mwanamke huyo atakapotibiwa na kupewa fomu ya polisi ya P3.

 

You can share this post!

Kwa nini tunapinga BBI

KEMUNTO: Mama Kayai chanzo chake katika uigizaji