• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Mwanamke apata jeneza nje ya nyumba yake Juja

Mwanamke apata jeneza nje ya nyumba yake Juja

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Riuriro eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, wameachwa na mshangao baada ya jeneza bila maiti kutupwa nje ya nyumba ya jirani wao mnamo Jumatano.

Mwanamke anayeishi peke yake alipata jeneza likiwa limeegeshwa nje ya mlango wake wa nyumba.

Mama huyo ambaye hakutaka kujitambulisha kwa sababu ya usalama wake alisema jambo hili lilimshtua ajabu huku akiwajulisha majirani wake.

Kulingana na mama huyo, alihamia katika kijiji hicho hivi majuzi lakini anashuku kuna watu wanaomuandama.

“Nina hofu tele kwa sababu sijui nianzie wapi. Sijui nilikosea nani, lakini hata hivyo sitatishika na nitaendelea kuishi hapa bila wasiwasi,” alijitetea mama huyo.

Alisema wale wanaomuonea uwivu amewaachia Mungu na hakuna wakati atatoka katika boma lake.

Alisema jeneza hilo lilikuwa na ujumbe wa kuogofya. Juu ya sanduku hilo kilikuwa na maandishi.

Kulingana na mwanamke huyo, maandishi ni, “Jiandae na jihadhari tutakukujia wakati wowote.”

Baada ya habari hizo kuenea katika kijiji hiyo wakazi wa eneo hilo waliachwa vinywa wazi huku wakishindwa lengo la wahuni hao kuleta sanduku hilo katika boma la mama huyo.

“Mimi sijui kama niko na maadui, sikumbuki kama hata nimekosana na mtu yeyote kwa siku za hivi karibuni,” alijitetea mama huyo aliyeonyesha hofu tele usoni mwake.

Hata hivyo polisi walifika katika kijiji hicho na kuchukua jeneza hilo hadi kituo cha polisi huku uchunguzi ukiendelea.

Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Juja, Bi Dorothy Migarusha alisema tayari wanaendelea na uchunguzi ili kubainisha chanzo cha tukio hilo.

“Hata sisi kama idara ya usalama tumeshindwa kueleza jinsi tukio kama hilo limeweza kutendeka kwa mama kama huyo,” alisema afisa huyo.

Tayari uchunguzi umeanzishwa kupitia idara ya upelelezi ili kubainisha chanzo cha tukio hilo.

Mama huyo alisema yeye haogopi kifo na watu hao wenye nia mbaya wafanye wapendalo.

“Mimi yote nimeachia Mungu; anayetaka kunidhuru ni shauri yake naamini maombi yangu yataniokoa,” alijitetea mama huyo.

Wakazi wa kijiji hicho wanaitaka serikali iweke usalama wa saa 24 kwa sababu kitendo hicho ni hatari kwa usalama.

Baada ya jeneza hilo kupelekwa kituo cha polisi cha Juja wakazi wa Riuriro walibaki na wasiwasi huku wakinong’onezana kwa sauti ya chini kuhusu tukio hilo la kuogofya.

Wakazi hao kwa kauli moja wamekubaliana kushirikiana kila mara pamoja ili kuzuia matukio ya aina hiyo mara nyingine.

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Kilimo cha mananasi kimemjenga hadi sasa ana...

Wakazi Kwale washauriwa kuzingatia njia bora za ukulima ili...