Mwanamke ataka mahari ya Sh700,000 ilipwe kesi ya talaka ikifaulu
MWANAMKE anayetaka kuvunja ndoa yake na mfanyabiashara Mpakistani, anataka mahakama ya Kadhi jijini Nairobi iamuru mwanamume huyo alipe salio la mahari la Sh700,000 wakati talaka itakapopitishwa.
Amedai kuwa, anataka kuvunja ndoa hiyo kutokana na mumewe kukosa uaminifu na kumtelekeza.
Ikiwa ombi hilo litafaulu, mfanyabiashara huyo huenda akaagizwa kulipa salio la mahari la Sh700,000, ambalo mwanamke huyo anadai baada ya ndo yao kuvunjwa.
Wawili hao walioana chini ya sheria za Kiislamu mwaka wa 2021 lakini hawajajaliwa kupata mtoto.
Mwanamke huyo analalamika katika hati zake mahakamani kwamba tangu walipofungishwa ndoa, mumewe alimwacha, kumpuuza na kushindwa kumtunza.
“Ameniweka katika nyumba ya mke mwenzangu. Amenitelekeza na hivyo kuninyima haki yangu ya ndoa,” alisema.
Mwanamke huyo pia amemshutumu mume huyo kwa kujiunga na Madhehebu ya Shia ambayo anadai yanagongana na imani yake ya kuwa Muislamu wa Sunni.
“Ananikosea heshima. Alileta kahaba kwenye nyumba yetu. Pia, ananiletea matusi machafu akiniita kahaba,” mwanamke huyo akasema.
Kulingana na mwanamke huyo, juhudi na hatua zote ambazo zimechukuliwa na jamaa zao kusuluhisha tofauti kati yao hazijazaa matunda.
“Kwa sababu ya tofauti zisizoweza kubatilishwa, ndoa yetu imevunjika zaidi ya kurekebishwa. Ombi hili halijaletwa kwa kushirikiana au kwa ushirikiano na mshtakiwa au na mtu mwingine yeyote anayehusika kwa njia yoyote na suala hili,” alisema.
Mwanamke huyo pia anataka malipo ya matunzo yaliyosalia.
Mumewe ambaye anatambulika mahakamani kama SAU bado hajaweka majibu katika kesi hiyo.
Iwapo atachagua kutojibu au kukubaliana na ombi hilo, mahakama hiyo ya Kiislamu itaendelea kusikiza kesi hiyo na kuvunja ndoa hiyo.
“Iwapo utashindwa kufika mahakamani tarehe na muda uliotajwa katika kesi hiyo, kesi itawekwa kwa ajili ya kusikilizwa na utapewa taarifa ya kusikilizwa,” stakabadhi za mahakama zinasema.
SAU ana siku 15 za kuwasilisha majibu yatakayotoa mwelekeo wa kesi hiyo.