Mwanamkwe akiri kusingizia mumewe unajisi baada ya kumtelekeza
MWANAMKE mmoja mjamzito mwenye umri wa miaka 35 kutoka Baringo Kaskazini alishangaza korti baada ya kukiri kuwa alidanganya kuwa mumewe alimnajisi binti yao wa miaka minane.
Mama huyo wa watoto wawili alishangaza Mahakama ya Kabarnet siku ya Jumatatu baada ya kukiri kuwa alifanya hiyo njama kama njia ya kulipiza kisasi kwani mumewe alimtelekeza.
Akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Edwin Mulochi, mwanamke huyo aliambia Mahakama kuwa mumewe alimtelekeza yeye na watoto na akaenda kuishi kwa mke wake wa kwanza.
Alisema hilo lilimkasirisha na hivyo akaamua kumsingizia makosa.
“Nilikasirishwa sana na kitendo cha mume wangu kutelekeza majukumu yake. Binti yangu alipolalamika kuhusu kuumwa na tumbo wiki kadhaa zilizopita, niliona fursa na nikamdanganya daktari kwamba binti yangu alidhulumwa kimapenzi na babake,” mwanamke huyo aliambia Mahakama.
“Namuomba Mungu na Mahakama hii anisamehe kwa sababu nilikuwa nalemewa na majukumu mengi nyumbani na nilitaka kumwadhibu mume wangu. Sikutarajia kwamba angekamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.
Kufuatia ufichuzi wake, upande wa mashtaka uliagiza akamatwe na kushtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo.
Kukiri kwa mama huyo kulijiri baada ya bintiye kuambia mahakama kuwa hajawahi kunajisiwa na babake na kwamba kesi yake ilibadilishwa baada ya kupelekwa katika kituo cha afya baada ya kulalamikia kuumwa na tumbo.
Wakati wa kuhojiwa na wakili wa serikali, Bi Rebecca Bartilol, mtoto huyo alidai kuwa analala kitanda kimoja na wazazi wake na hakuna wakati ambapo baba yake alimnajisi.
“Nilipelekwa hospitalini baada ya kulalamika kuumwa na tumbo lakini baadaye ikabadilishwa. Baba hakunifanyia kitu (Baba yangu hakuwahi kunifanyia lolote),” aliambia mahakama.
Mahakama ilielezwa kwamba kando na kumwambia bintiye adanganye, mwanamke huyo pia alirekodi taarifa za uongo katika kituo cha Polisi cha Kabarnet kabla ya kuwahusisha maafisa wa idara ya watoto na wanaharakati wa haki za binadamu.
Mwendesha mashtaka alisema kufuatia mwanamke kukiri makosa hayo, kesi hiyo itafungwa na mshtakiwa aachiwe huru bila masharti.
“Ikiwa tutaendelea kumshikilia mshtakiwa, kwa msingi wa uongo itakuwa dhuluma kubwa. Ninaomba kesi hii ifungwe na mtuhumiwa aachiwe huru bila masharti,” alisema Bi Bartilol.