Habari Mseto

Mwanamume adaiwa kuingiza mfukoni Sh4m za kampuni akidai atawaletea sukari

April 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA ameshtakiwa kuilaghai kampuni Dola za Marekani (USD) 103,000 (Sh4,120,000) akidai anauza sukari.

John Bosco Olago aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Bernard Ochoi alikana shtaka na kuahidi kuilipa kampuni ya Hainan Rui Rong Long International Trading Limited pesa alizochukua kwake.

Shtaka lilisema kati ya Novemba 24, 2023 na Feburuari 28, 2024 katika eneo la Kilimani Kaunti ya Nairobi alipokea USD 103,000 (KSh4,120,000) akiwa na nia ya kutapeli kampuni ya Hainan Rui Rong Long International Trading Limited.

Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka James Gachoka kwamba Olago alipokea pesa hizo akidai alikuwa na uwezo wa kuiuzia kampuni hiyo tani 1,000 za sukari.

“Lakini kumbe ulikuwa uwongo,” Bw Ochoi alijuzwa na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa Bw Gachoka.

Akiomba aachiliwe kwa dhamana mshtakiwa alikiri alipokea pesa hizo lakini akasema “majadiliano yanaendelea kati yake na Hainan Rui Rong kulipa pesa hizo alizopokea.”

Olago aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “ameoa na yuko na mke na watoto na hawezi kutoroka”

Aliongeza kueleza mahakama kwamba itabidi alipe pesa hizo kudumisha biashara na jina la kampuni yake.

Olago aliongeza kusema kama mfanyabiashara mwenye heshima atahakikisha amefika kortini kutunza jina la kampuni yake na pia yeye mwenyewe.

Bw Ochoi alimwachilia kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa tasilimu au dhamana ya Sh3 milioni.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 18,2024 kutengewa siku ya kusikizwa.