Habari Mseto

Mwanamume aliyeishi kisimani kwa siku 13 aokolewa

June 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA ALEX NJERU

MWANAMUME mwenye akili punguani katika kijiji cha Gatituni eneo la Chuka, Kaunti ya Tharaka Nithi ameshangaza dunia aliibuka akiwa hai baada ya kuishi ndani ya kisima cha futi 60 kwa siku 13 bila chakula.

Bw Royford Mugambi, 42, alitolewa kwa kisima hicho hapo Jumatano jioni, huku umati ukikusanyika kushuhudia kisa hicho kisicho ch akawaida.

Mwanamume anayeishi na mamaye mkongwe, alitoweka asubuhi ya Mei 22 mwaka huu.

Akisema na wanahabari nyumbani kwao Alhamisi, Bw Henry Gitonga, ambaye ni nduguye Bw Mugambi, alisema kuwa wamekuwa wakimsaka ndugu yao tangu alipopotea, hadi katika mochari ya Hospitali ya Kaunit ya Chuka.

Familia hiyo ilipiga ripoti kuhusu kutoweka kwake katika Kiuto cha Polisi cha Chuka na walikuwa wameanza kukata tamaa wakati alipatikana katika kisima hicho.

Bw Gitonga alisema jirani yao, Bw John Mwenda, alikuwa alifanya kazi shambani karibu na kisima hicho aliposikia mtu akimwita na kukisia alikuwa babaye aliyekuwa akifanya kazi mita chache kutoka hapo. Lakini babaye alisema hakuwa amemwita.

Bw Mwenda aliendelea na kazi yake lakini akasikia sauti hiyo tena. Raundi hii, mtu huyo alimuita kwa jina lake na lipotafuta ilikotokea sauti hiyo, aligundua kuwa aliyemuita alikuwa ndani ya kisima na sauti yake aliifahamu. Ilikuwa ya Bw Mugambi.

Alikimbia kuchhukua ngazi, akaifunga kwa kamba na kuiteremsha kwa kisima hicho. Kisha alimwambia Mugambi kushikilia ngazi hiyo kwa nguvu huku wakazi wakimvuta nje.

Alipotoka nje, Bw Mugambi aliomba maji ya kunywa. “Mwili wake ulionekana kukosa nguvu huku akiwa amechanganyikiwa,” alisema.