• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Mwanamume apatikana amefariki katika hali tatanishi Githurai 45

Mwanamume apatikana amefariki katika hali tatanishi Githurai 45

Na SAMMY WAWERU

MWANAMUME mmoja eneo la Githurai 45, Kiambu asubuhi ya kuamkia Jumanne amepatikana amefariki katika hali isiyoeleweka baada ya kudaiwa kunywa pombe hatari.

Kulingana na wapangaji wa ploti anayoishi mwanamume huyo aliyetambulika kama Mwaniki na ambaye alikuwa akichuuza maji, Jumatatu usiku alifika akiwa mlevi kupindukia ingawa alikuwa akijifahamu.

“Alikuwa na fahamu lakini hakuweza kuzungumza. Tumemzoa kufika akiwa mlevi,” amesema mama ambaye ni jirani yake.

Mwili wa mwanamume aliyepatikana amefariki mtaani Githurai 45 Jumanne asubuhi baada ya kudaiwa kunywa pombe yenye sumu, ukisafirishwa kwa gari la kituo cha polisi cha Kimbo, Ruiru, kaunti ya Kiambu.
Picha/ Sammy Waweru

Mwili wake ulikuwa mita chache kutoka nyumba anayoishi, funguo zikiwekelewa kifuani. Simu yake ya mkono haikupatikana, mfukoni akiwa na kalamu na kitabu kilichosemekana ni cha kusajili wenye deni la maji. Mchuuzi mwenzake amesema kwamba mwendo wa saa nne za usiku kabla ya kuaga dunia alilalamika kuhusu maumivu ya tumbo.

“Alinieleza anahisi maumivu ya tumbo akidai kutiliwa kinywaji kikali,” alisimulia.

Akithibitisha kisa hicho, afisa mmoja wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kimbo, Ruiru, aliyejitambulisha tu kama Bw Kiiru amesema huenda mwanamume huyo alifariki kutokana na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Uchunguzi waanzishwa

Hata hivyo, alisema uchunguzi umeanzishwa mwili wake ukipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, KU.

Baa alimokuwa akinywa pombe haijabainika kufikia sasa.

Unywaji wa pombe katika kaunti ya Kiambu umekuwa kero kuu, gavana Ferdinand Waititu na mbunge mwakilishi wa wanawake Gathoni Wa Muchomba wakiendesha kampeni dhidi yake. Mwanzoni mwa 2018, Bw Waititu alikomesha maafisa wa polisi kutoa leseni za kuhudumu kwa wamiliki wa baa.

Gavana alisema awali maafisa hao walishiriki katika utoaji wa leseni hizo, lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyoshuhudiwa katika kampeni dhidi ya pombe, hasa ile haramu Kiambu.

Afisi yake ndiyo ilichukua jukumu hilo kuona iwapo kutakuwa na mabadiliko.

  • Tags

You can share this post!

AUNTY POLLY: Rafiki anidhalilisha mtandaoni, nisaidie

UREMBO: Jinsi unavyoweza kuitunza ngozi yako

adminleo