Mwanamume asakwa kwa mauaji ya babake
Na NDUNGU GACHANE
POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanamsaka mwanamume anayeshukiwa kumuua babake na kuutupa mwili mtoni katika kijiji cha Muthithi, eneobunge la Kiharu.
Wilson Mamwea, mwenye umri wa miaka 35, anadaiwa kumuua babake, Peter Njoroge, mwenye umri wa miaka 69 mnamo Ijumaa usiku na kuutupa mwili wake katika Mto Maragua, ulio karibu na boma yao.
Mamake mshukiwa tayari amekamatwa na polisi ili kusaidia katika uchunguzi.
Jamaa za marehemu na wakazi waliupata mwili huo kutokana na matone ya damu yaliyoelekea mtoni. Mwili wake ulikuwa na majeraha ya shingo na kichwa.
Jane Wangari, ambaye ni mwanawe marehemu, alisema kwamba kakake amekuwa akitishia kumuua babake.
Alisema kuwa familia hiyo ilikuwa ikikumbwa na mzozo wa ardhi, lakini serfikali iliingilia kati ambapo kila mmoja wao aligawiwa sehemu yake.
“Babangu na kakangu hawajakuwa na uhusiano mwema. Alimuua baada yao kuachwa wakiwa wawili nyumban,” akasema.
Majirani walimlaumu mshukiwa kwa kutumia mihadarati, wakisema kuwa athari zake ndizo zilimfanya kutekeleza mauaji hayo.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi katika kaunti hiyo Mohammed Farah alisema kuwa mamake mshukiwa amekamatwa ili kuwasaidia katika uchunguzi.
Alisema kuwa atawasaidia kubaini chanzo cha mauaji na ikiwa alishiriki katika mauaji ya mumewe.
“Tunamzuilia mkewe marehemu ili kubaini ikiwa alihusika katika mauaji hayo au la. Ikiwa tutathibitisha kwamba hana hatia yoyote, tutamwachilia,” akasema.
Alieleza kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha ya kichwa, yanayoaminika kusababishwa na kifaa butu.
“Tungali hatujajua hasa kilichomfanya mshukiwa kufanya kitendo hicho dhidi ya babake mzazi,” akasema Bw Farah.
Aliwaomba wakazi kuwasaidia polisi kumkamata mshukiwa, ambaye alitoroka mara tu baada ya kisa hicho.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti ya Murang’a ili kufanyiwa upasuaji.
Wakazi waliojawa na hasira waliichoma nyumba ya mshukiwa, wakiapa kumkabili akirejea.
Visa vya mauaji na utekanyinyara vimeongezeka sana katika eneo hilo, hali ambayo imezua hofu miongoni mwa wakazi kuhusu hali ya usalama.