• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mwanamume auawa kinyama Gatundu Kaskazini

Mwanamume auawa kinyama Gatundu Kaskazini

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kawira eneo la Gatundu Kaskazini, wamelalamika vikali baada ya mwenyekiti wao wa Nyumba Kumi kuuawa kinyama.

Wakazi hao wameandamana katika kijiji hicho huku wakitaka serikali kuingilia kati na kuwanasa wahalifu wote waliotekeleza kitendo hicho.

Wakazi hao walidai kuwa Bw Peter Kanja aliuawa kinyama na watu wasiojulikana mnamo Jumatatu usiku.

Bi Mary Wanjiru ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amesema mwendazake alihadaiwa na watu wasiojulikana halafu baadaye akauawa bila kutarajia.

“Sisi wakazi wa hapa Kawira tulimheshimu marehemu kwa kazi nzuri aliyotufanyia kama wanakijiji. Alikuwa mtu mnyenyekevu aliyeshirikiana kwa uzuri na wakazi wa kijiji hiki,” amesema Bi Wanjiru.

Ameitaka serikali ichukue hatua ili waliohusika wafunguliwe hatua za kisheria kwa kushtakiwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Alisikitika wahalifu wamekuwa wengi miongoni mwa wananchi.

Bi Judy Wanjiku ambaye ni dadake marehemu alisema wao kama familia wamesikitishwa sana na kitendo hicho cha unyama kilichotendwa na wahalifu hao.

“Sisi kama familia tumehuzunishwa sana kwa kupoteza mmoja wetu ambaye alijitolea mhanga kufanya kazi yake bila uoga wowote. Kitendo hicho ni kama kilipangwa ili auawe kwa sababu alikuwa mstari wa mbele kukemea maovu yaliyotendeka kijijini,” amesema Bi Wanjiku.

Ameiomba serikali ijitokeze wazi na kuangamiza pombe haramu inayoendelea kubugiwa na vijana wengi eneo hilo.

“Sisi kama wakazi wa hapa Kawira tumeachwa na wasiwasi kwa sababu ya wengine wetu kuuawa kiholela bila sababu yoyote. Serikali iingilie kati kukabiliana na maovu mengi yanayokumba watu eneo hili,” amesema Bi Wanjiku.

Wakazi hao wamesema wahalifu hao hawastahili kukaribia mahali wakazi wa kijiji hicho wapo.

You can share this post!

Njiraini amezea mate kiti cha Swazuri

Waluke amwomba Tuju msamaha

adminleo