Mwanamume kulipa MCA Sh20 milioni kwa kumchafulia jina Facebook
CHAPISHO la Facebook litamgharimu mwanamume Sh20 milioni baada ya jaji kuamua kuwa maneno aliyotumia yalikuwa ya kuharibia mtu jina.
Michael Oduory, anayejulikana pia kama Mike Ochieng’, huenda alichapisha maneno hayo kwa mzaha, lakini Jaji wa Mahakama Kuu David Kemei aliamua kuwa yalilenga kumharibia jina mlalamishi.
“Kitendo cha mshtakiwa (Bw Oduory) kuchapisha kilionyesha nia mbaya, na mshtakiwa alionyesha uzembe kwa kutofanya juhudi kuthibitisha ukweli wa madai hayo,” alisema jaji.
Mlalamishi Bw Washington Bonyo, anayejulikana pia kama Dasani, ambaye ni Mwakilishi Wadi katika Bunge la Kaunti (MCA) Kaunti ya Siaya, alimshtaki Bw Oduory kwa chapisho hilo, akisema yalikuwa ya kumpaka tope.
Mahakama iliambiwa kuwa Bw Oduory alidai katika chapisho hilo kuwa MCA huyo alikuwa amenyakua mke wa mtu mwingine.
Chapisho hilo liliambatishwa na picha pamoja na chapisho lingine lililodai kuwa mume wa mwanamke huyo “alimlilia” Bw Oduory ili afichue tabia ya MCA huyo.
Baadhi ya maneno yalichapishwa kwa lugha ya Kijaluo.
Jaji aliamua kuwa baada ya kutakiwa kuondoa madai, Bw Oduory alikataa kufuta machapisho hayo na kuomba msamaha, hali iliyomlazimu Bw Bonyo kupeleka suala hilo mahakamani.
Bw Bonyo alisema kuwa machapisho hayo, moja baada ya jingine na kwa ujumla, yaliwafikia watumiaji wengi wa Facebook, yakasambazwa, kunukuliwa na hata kupendwa kwenye kurasa za Facebook za watu wengine.
MCA huyo alisema kuwa machapisho hayo yalikuwa wazi kwa mtu yeyote ulimwenguni, na bado yalipatikana mtandaoni licha ya kumtaka Bw Oduory kuyafuta.
Alisema kuwa machapisho hayo yalimsababishIa dharau, kejeli na fedheha, na kwa yeyote mwenye fikra timamu, yalifanya aonekane kama mtu msherati na asiye na maadili.
Bw Bonyo aliongeza kuwa machapisho hayo yalimsawiri kama mtu mwenye tabia za kutiliwa shaka, asiye na sifa za kushikilia wadhifa wa umma, na pia mtu mdanganyifu na mfisadi.
Bw Oduory, kwa upande wake, alikanusha kuwa ndiye aliyechapisha maneno hayo, akisema yeye ni mkazi wa Nairobi na si Siaya, na anamfahamu tu Bw Bonyo kama MCA.
Alisema huenda machapisho hayo yalifanywa na mpinzani wa kisiasa wa mlalamishi, lakini hakika hayakutoka kwake kwa kuwa yeye si mwanasiasa.
Aidha, alisema kuwa kesi hiyo ilimshangaza kwa sababu hajawahi kukiuka sheria.
Jaji alisema kuwa ushahidi wa Bw Bonyo haukupingwa kwa kuwa Bw Oduory aliwasilisha tu hati ya kujibu mashtaka na utetezi, lakini hakutoa ushahidi wa kupinga madai yaliyoletwa mahakamani.
Mbali na fidia ya Sh20 milioni, mahakama ilimwagiza Bw Oduory amuombe radhi Bw Bonyo na afute machapisho hayo.
Jaji alielekeza kuwa msamaha huo upewe nafasi kubwa zaidi kupitia mtandao huo wa kijamii.