'Mwanamume mla kombamwiko'
Na MARY WANGARI
MWANAMUME mmoja jijini Nairobi huwafanya kombamwiko kitoweo chake.
Geoffrey Lugai mkazi wa eneo la Soweto, Kibera, jijini Nairobi, anaeleza jinsi anavyoandaa kitoweo cha mende anaowafuga nyumbani kwake.
“Nilianza kula mende miaka minne iliyopita. Huwa nachukua tepu na kuibandika kwenye ukuta ambapo mende huja na kukwama hapo. Kisha mimi huwachukua na kuwatia kwenye maji kabla ya kuwakaanga kikaangioni,” akasema Lugai alipohojiwa na runinga ya NTV.
“Ni chakula kitamu kama kumbikumbi. Mende hustahimili mazingira magumu kwa muda mrefu ikiwemo mabomu ya nyuklia,” anasema huku akitafuna mende na kuchanua tabasamu.
Kulingana na msanii huyu wa uchoraji, uraibu wake unatokana na kwamba mende ni wadudu wakakamavu ambao wanaweza kustahimili hali ngumu na anasema wana uwezo wa kusaidia kuimarisha kinga mwili.
Kisa cha Lugaye kinajiri huku Wakenya wakiwa na wasiwasi kufuatia ripoti kwamba wauzaji nyama hutumia kemikali hatari ili kuhifadhi nyama kwa muda mrefu zaidi; hasa katika madukamakuu.
Mnamo Alhamisi, Waziri wa Afya, Sicily Kariuki, alisema kati ya sambuli 40 za nyama ya ng’ombe zilizochukuliwa katika maduka, ni sita zilizopatikana kuwa na kiwango cha juu kupita kiasi cha kemikali aina ya Sodium bisulfite iliyotumika katika kuhifadhi bidhaa hiyo.
Idadi hiyo inawakilisha asilimia 15.
Aidha, dukakuu la Naivas mnamo Alhamisi lilisitisha uuzaji wa nyama katika matawi yake kote nchini.
Habari hii imeandaliwa baada ya kutazama taarifa ya makala yaliyopeperushwa na runinga ya NTV mnamo Jumatano