Mwanamume taabani kwa kujifanya mkewe Ruto
Na RICHARD MUNGUTI
MWANAUME aliyejifanya kuwa Bi Rachel Ruto, mkewe Naibu wa Rais William Ruto amezuiliwa kwa muda wa siku tatu kuhojiwa katika kituo cha polisi cha Central, Nairobi.
Bw Michael Mito Atito (pichani) alikamatwa na maafisa wa polisi wa kupambana uhalifu wa kimitandao alipofungua akaunti ya Facebook akijifanya kuwa Bi Rachel Ruto na kuanza kuomba misaada kuwasaidia maskini.
Bw Atito anadaiwa alifungua akaunti ya Facebook na kubandika picha ya Bi Rachel Ruto na kuomba msaada wa kifedha utumwe kwa njia ya M-Pesa.
Katika ujumbe aliotuma mshukiwa huyo wa uhalifu wa kimitandao alifafanua kuwa anahitaji pesa hizo kuandikisha malori kwa msijali wa magari katika Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi (NTSA).
“Naomba wahisani wanitumie pesa kusajili malori niliyionunulia watu kutoka jamii maskini katika afisi ya msajili wa magari katika afisi za NTSA,” alisema Bw Atito katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa Facebook.
Afisa anayechunguza kesi hii alimweleza hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani, Nairobi Bi Muthoni Nzibe kwamba mshukiwa huyo atafunguliwa mashtaka pamoja na mshukiwa mwingine ambaye anazuiliwa.
“Nahitaji muda wa kuwatia nguvuni washukiwa wengine sawia na huyu ili kumhoji Bw Atito,” Koplo George Chai alimweleza Bi Nzibe jana kortini.
Pia Koplo Chai aliambia mahakama anahitaji kupokea taarifa za akaunti ya M-Pesa ya mshukiwa huyu (Atito) kubaini pesa alizopokea kwa ajili ya mradi huo wa ‘kufaidi maskini’ wa Bi Ruto.
Akitoa uamuzi Bi Nzibe aliamuru Bw Atito azuiliwe hadi Februari 7.
Akasema Bi Nzibe , “Hii mahakama imetilia maanani mawasilisho ya afisa huyu wa polisi na kufikia uamuzi anahitaji kuruhusiwa kukuhoji kwa muda wa siku tatu.”
Hakimu alisema madai dhidi ya mshukiwa ni mazito na polisi wanahitaji kupewa muda kukamilisha mahojiano.