Habari Mseto

Mwanamuziki Sammy Irungu sasa kuanzisha kanisa lake

January 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MWANAMUZIKI wa nyimbo za injili kwa lugha ya Kikikuyu, Sammy Irungu, sasa ametangaza mpango kwa kuanzisha kanisa.

Mwanamuziki huyo anaonekana kuiga mkondo ambao umekuwa ukifuatwa na watu maarufu (celebs) kutoka eneo la Mlima Kenya, ambao wamekuwa wakitumia umaarufu wao kuanzisha makanisa yao binafsi.

Bw Irungu, anayefahamika kwa nyimbo maarufu kama ‘Niwikite Magegania’ (Umefanya Maajabu), ‘Ndukanjethe’ (Usinitafute), ‘Maguta Mari Thina’ (Upako una Uchungu) kati ya nyingine nyingi, alitangaza mpango huo Ijumaa, Januari 19, 2024 akisema “wakati wake umefika kukumbatia njia nyingine ya kueneza injili.”

Kwenye mahojiano, Bw Irungu alisema kuwa baada ya kuwa katika sekta ya uimbaji wa nyimbo za injili kwa zaidi ya miaka 15, wakati umefika kwake “kukubali sauti ya Mungu kuingia katika uhubiri”.

“Nilipata mwito wa kuingia kwenye uhubiri 2020. Hata hivyo, nimekuwa nikiahirisha utimizaji wa mwito huo. Mungu amekuwa akizungumza nami. Nadhani wakati umefika,” akasena Bw Irungu.

Ijapokuwa hajatangaza rasmi jina la kanisa hilo, alisema kuwa ibada ya kwanza itaanza katika Hoteli ya Blue Springs, iliyo katika Bababara Kuu ya Thika, Januari 26, 2024.

“Nawaalika mashabiki wangu wote kujiunga nami kwenye safari hii mpya nimeanza. Nahisi kuwa, baada ya kuwa kwenye tasnia ya uimbaji wa nyimbo za injili kwa zaidi ya miaka 15, wakati umefika nimtumikie Mungu kwa njia nyingine tofauti,” akasema mwanamuziki huyo.

Tangazo lake linaonekana kufuata mkondo ambao umekuwa ukiigwa na watu maarufu kutoka ukanda wa Mlima Kenya kuanzisha makanisa yao binafsi.

Baadhi ya ‘macelebs’ ambao wameanzisha makanisa yao ni mcheshi Benson Gathungu, maarufu kama ‘Muthee Kiengei’, ambaye miezi michache iliyopita alianzisha kanisa la Jesus Christ Compassion Ministries (JCM).

Wahubiri na wanamuziki wengine wanaoendesha makanisa yao ni Bishop JJ Gitahi (anayeendesha kanisa la Priesthood), Askofu na Mcheshi Paul Kuria (anayeendesha kanisa la Joy Centre), wanamuziki Isaac Kahura, Elijah Miller kati ya wengine wengi.