Habari Mseto

Mwaniaji aliyetishia kumuua diwani Makueni atupwa jela miaka miwili

May 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

MWANIAJI kiti cha udiwani wadi ya Kiteta Kisau katika Kaunti ya Makueni amesukumwa jela miaka miwili bila faini kwa kutishia kumuua diwani Dennis Kioko Mainga.

Dennis Wambua Masavu alifungwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Zainab Abdul aliyempata na hatia ya kumtishia maisha Bw Mainga.

Bi Abdul alisema Masavu aliapa kwamba ama yeye ama Bw Mainga “atakufa.”

“Siwezi kushindwa kiti cha udiwani kisha niagizwe nilipe gharama ya Sh1 milioni. Ama mimi nitakufa ama diwani afe,” Masavu aliapa alipohutubu.

Hakimu alisema matamshi hayo hayawezi kuchukuliwa kwa wepesi kwa vile Masavu alimtishia maisha mpinzani wake kisiasa.

“Upande wa mashtaka umethibitisha kwamba Masavu alitisha kumuua Bw Mainga baada ya kumshinda katika kinyang’anyiro cha wadi ya Kiteta/Kisau Mbooni Mashariki katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022,” Bi Abdul alisema.

Mahakama ilisema mashahidi saba waliofika kortini walithibitisha kwamba Masavu alitamka maneno hayo mara tatu alipohutubia kikao cha familia, wakati wa sherehe ya ndoa na alipohutubia vijana sokoni.

Mahakama ilielezwa katika mkutano huo wa familia kwamba Masavu alilalamika kwamba alishindwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo kwa vile watu 23 wa familia walikosa kumpigia kura.

Baada ya kushindwa, mshtakiwa aliwasilisha kesi katika mahakama ya Tawa.

Mahakama hiyo ya kuamua kesi za uchaguzi ilitupilia mbali kesi hiyo na kumwagiza Masavu “alipe gharama ya kesi Sh1 milioni.”

“Baada ya kutathmini ushahidi wote, nimefikia uamuzi kwamba mshtakiwa alimtishia maisha diwani Mainga na yuko na hatia kama alivyoshtakiwa,” Bi Abdul alisema.

Alimfunga miaka miwili jela na kumpa siku 14 kukata rufaa.