• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
Mwathiriwa mwingine wa mlipuko wa gesi Embakasi afariki dunia

Mwathiriwa mwingine wa mlipuko wa gesi Embakasi afariki dunia

MWATHIRIWA wa 12 wa mlipuko wa gesi uliotokea Embakasi Ijumaa usiku, aliaga dunia katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, siku moja baada ya kuhojiwa na Taifa Leo.

Maria Nyangige, ambaye alikuwa mama wa watoto wawili, alikuwa amehojiwa na Taifa Leo mnamo Jumatano kuhusu ahadi hewa ambazo walikuwa wamepewa na serikali.

Mhanga huyo alikuwa muuzaji wa mboga na vitafunio katika mtaa wa Mradi ambapo mlipuko ulitokea mnamo Februari 1, 2024.

Mwanawe, Bw Peter Chacha, alithibitisha kutokea kwa kifo cha mamake Ijumaa jioni.

Wakati ambapo mlipuko huo ulitokea, Maria alikuwa anaelekea nyumbani baada ya kazi ya mchana kutwa.

Alikuwa amemaliza kukanda unga wa kupika vitafunio wakati ambapo mlipuko huo ulitokea na moto ukawaka kila mahali.

Mlipuko huo ulisababisha wingu la moshi kutanda kotekote huku kila mtu akikimbilia usalama lakini wapi!

Wakati wa mahojiano, Maria alikumbuka jinsi ambavyo mwili wake ulifunikwa motoni na uchungu ambao ulikuwepo.

Alisimulia kuwa uchungu huo ulikuwa mwingi kiasi kuwa hangeweza kutembea.

Alichomeka kuanzia kwa shingoni hadi miguuni na maisha yake yakabadilika na kusambaratika kabisa.

Yeye ndiye aliyetegemewa lakini alilemewa na madeni na kukosa kutimizia familia yake mahitaji mengine kama kodi na karo ya shule baada ya ajali hiyo.

Alisema wakati mwingine watoto wake walikuwa wakilala njaa ilhali wakati ambapo alikuwa buheri wa afya, mambo yalikuwa yamemnyookea.

Wakati mahojiano, alikosa hata chakula na pesa za kununua tembe za kupunguza maumivu. Kwa kuwa sasa hayuko, hatima ya watoto wake haijulikani.

Kwa mujibu wa jirani yake Phillip Wafula, Maria alikuwa mwanamke ambaye alikuwa na bidii huku akisaka riziki kwa familia yake.

Siku mbili zilizopita, akiwa amesononeka Maria alikuwa na shaka ikiwa angewahi kupona.

Alisikitika iwapo maisha yake nayo yangerejea kama kawaida.

“Sijui ni kwa kipindi kipi nitasalia hivi kabla ya kupona hata kama nitapata maisha yangu kama kawaida,” akasema.

“Kabla ya moto, nilikuwa mzima wa afya na sikuwahi kufikiria familia yangu ingelemewa na mahitaji ya kimsingi,” aliongeza wakati huo.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja aagiza pombe ya makali kuondolewa kwa steji za matatu

Diamond Platnumz aelekea ‘Zenji’ kumuomba Zuchu...

T L