Mwili wa aliyekuwa mkuu wa polisi wazikwa baada ya miaka 5
Na Paul Mutua
Mwili wa aliyekuwa mkuu wa polisi katika Kaunti ya Nairobi, Timothy Mwandi Muumbo, ulizikwa Jumamosi miaka mitano baada ya kifo chake.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na watu wachache wa familia yake yalifanyika kijiji cha Nzatani, Migwani, Mwingi Magharibi Kaunti ya Kitui ambako mkewe wa kwanza Phiatah alizikwa miaka saba iliyopita.Mwili huo umekuwa mochari familia ya mke wa kwanza ikizozana na ya mke wa pili.
Wakati wa mazishi, mwanawe wa kwanza, Mwinzi Muumbo na kitinda mimba wa mke wa pili, Billy Mbuvi, hawakuhudhuria. Jamaa wa familia ya marehemu alisema kwamba walifaulu kupata agizo la mahakama kuzika baba yao.
Akizungumza katika mazishi hayo, mwana wa marehemu , Alex Munyasya, alishukuru wote waliosimama na familia tangu kifo cha baba yao.
Kwa miaka mitano, familia ya Muumbo imekuwa ikizozana kuhusu alipopaswa kuzikwa huku baadhi ya wanawe wakitaka azikwe kando na kaburi la mke wa kwanza huku wengine wakitaka azikwe katika boma la mke wa pili Josephine Kiloko aliyezikwa Mbakini, Mwingi.
Kiini cha mzozo huo ni mali yake inayokisiwa kuwa ya thamani ya Sh1 bilioni. Mzozo huo ulikuwa kati ya wanawe Johnstone Kassim Mwandi, Alex na Carolyn kwa upande mmoja dhidi ya Mwinzi na Mbuvi.Gharama ya kuhifadhi mwili wake katika mochari ya Lee jijini Nairobi ilikuwa karibu Sh5milioni.