• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Mwili wa Collymore wachomwa

Mwili wa Collymore wachomwa

Na VALENTINE OBARA

MWILI wa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, marehemu Bob Collymore ulichomwa Jumanne kwenye mazishi yaliyohudhuriwa na watu wachache.

Mwili wake uliondolewa katika hifadhi ya maiti ya Lee jijini Nairobi dakika chache baada ya saa nne asubuhi na kupelekwa katika makaburi ya kuchoma miili ya wafu ya Kariokor.

Marehemu alisafirishwa kwenye msafara wa magari yaliyoongozwa na pikipiki za polisi na kuvutia umati makaburini, ambako kulikuwa na ulinzi mkali langoni.

Walinzi waliojumuisha polisi wa utawala wenye silaha, askari wa kampuni ya kibinafsi na walinzi wengine ambao walikuwa wamevaa kiraia, waliruhusu gari lililobeba mwili wa Bw Collymore kuingia moja kwa moja pamoja na magari mengine matatu ya kifahari.

Magari hayo yaliyoaminika kubeba jamaa zake wa karibu yalikuwa na vioo vyeusi na haingeweza kujulikana nani hasa alikuwa ndani.

Magari mengine yote yaliyofuata yalikaguliwa kwa makini zaidi na walinzi waliothibitisha kama waliokuwemo walikuwa kwenye orodha ya walioidhinishwa kuingia makaburini kabla yaruhusiwe kuelekea ndani.

Baadhi ya waliowasili walikatazwa kuingia ikiwemo ambulensi moja ya shirika la Kenya Red Cross, lakini ambulensi nyingine iliwasili baadaye na kuruhusiwa kuingia.

Kuna watu waliojaribu kubishana na walinzi ili waruhusiwe kuingia lakini hawakufua dafu.

Bw Collymore alifariki nyumbani kwake Jumatatu alfajiri kutokana na saratani ya damu.

Ijapokuwa mtindo wa kuchoma miili ya wafu haujakumbatiwa na wengi nchini kwa sababu za kitamaduni au kidini, siku za majuzi watu mashuhuri wamekuwa wakipendelea miili yao ichomwe wanapofariki.

Miongoni mwa Wakenya ambao walifanyiwa mazishi kwa njia hiyo inayotumiwa sana na Wahindi ni aliyekuwa mshindi wa tuzo la Nobel, Wangari Maathai, mwanasiasa mkongwe aliyepigania demokrasia Kenneth Matiba na Bi Mary Kuria ambaye alikuwa mke wa Askofu Mkuu Manasses Kuria wa Kanisa la Anglikana.

Jana, bodi ya Safaricom ilimchagua Bw Michael Joseph, ambaye alikuwa mtangulizi wa Bw Collymore kushikilia wadhifa huo kwa muda kabla afisa mkuu mpya wa kudumu aajiriwe.

You can share this post!

Everton kuwasili nchini Julai 6 tayari kulimana na...

Gavana aomba serikali yake ivunjwe

adminleo