Mzee jela miezi minane kwa kuiba marashi kufurahisha mpenzi
Na TITUS OMINDE
MZEE aliyekiri kuiba marashi katika supamaketi ili kumfurahisha mpenzi wake amehukumiwa na mahakama moja mjini Eldoret kifungo cha miezi minane jela.
Mahakama iliambiwa kuwa Mzee Alfred Lamasi, 64, aliiba marashi hayo aina ya ‘Army Signature’ katika dukakuu la Naivas tawi la Eldoret mwendo wa saa moja jioni mnamo Oktoba 11, 2019.
Upande wa mashtaka umeiambia mahakama kuwa marashi hayo yalikuwa yenye thamani ya Sh1,690 pesa taslimu.
Amekiri mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu mkazi Sylvia Wewa.
Wakati wa kujitetea kwake, ameiambia mahakama kuwa alikuwa anaugua ugonjwa wa pumu pamoja na kudai kuwa shetani ndiye alimdanganya hadi akatekeleza kitendo hicho cha wizi kwa nia ya kumfurahisha mpenzi wake.
Licha ya kujitetea kwake, hakimu huyo alionyesha kutoridhishwa na kauli yake.
“Nikiangalia umri wako, hauambatani na ulichokifanya asilani. Haya ni mambo ya vijana kuwafurahisha wapenzi wao. Kwa hivyo, mahakama inaweza kukuhurumia kwa kukupunguzia kifungo,” aliyasema hayo hakimu mkuu mkazi huku akimfunga miezi minane jela.
Kudondokwa machozi kwa mzee huyo mahakamani hakukuzuia mahakama kumlisha maharage jela kwa muda huo wa miezi minane.
Hata hivyo, mzee huyo alionekana kujutia matendo yake huku akitoa ahadi kwamba kutorudia.
Mzee huyo ameashiria kuwa atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Mahakama imempa siku 14 kukata rufaa hiyo.