Mzozo wa mabwawa wachacha maandamano yakinukia
BARNABAS BII na WYCLIFF KIPSANG
WAKAZI wa eneo la Kipsaiya katika kaunti ya Elgeyo Marakwet ambako bwawa la Arror litajengwa, sasa wanataka mradi huo usitishwe hadi uchunguzi kuhusu madai ya kupotea kwa zaidi ya Sh20 bilioni utakapokamilishwa.
Wakazi hao ambao walifanya maandamano jana katika barabara ya Iten-Kapsowar, walisifu juhudi za Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Bw George Kinoti za kuchunguza kupotea kwa pesa hizo ambazo zilidaiwa kulipwa kama mlungula.
“Huu mradi umezingirwa na usiri mwingi mno kwa sababu wananchi hawakushirikishwa katika maandalizi yake. Tunamuunga mkono Rais katika vita dhidi ya ufisadi,” akasema Bw Benjamin Cheboi, ambaye ni mkazi wa eneo hilo.
Wakazi hao ambao walikuwa wamebeba mabango walitaka viongozi fulani kutoka eneo hilo wakamatwe kuhusiana na sakata hiyo huku wakiapa kutohama kutoka mashamba hadi pale watakapolipwa fidia.
“Tulidhani mradi huu ulikuwa mzuri na ambao ungeimarisha uchumi wa eneo hili lakini sasa watu fulani walafi wameugeuza kuwa wao kujipatia utajiri wa haraka,” akasema, mkazi, Bw Amos Koech.
“Tumesikia viongozi wengine kutoka eneo hilo wakipiga kelele kuhusu suala hili. Ni nini wanajua? Wao pia walazimishwe kuandikisha taarifa kwa DCI. Inasikitisha kuwa viongozi wetu wanatumia ardhi yetu kujitajirisha,” mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina Mathew Yego akasema.
Wakati huo huo, Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), jana ilifichua kuwa haikupewa majina ya mashamba ambako familia 900 ambazo ardhi zao zilitwaliwa kwa ujenzi wa mabwawa mawili katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, zilifaa kuhamishiwa.
Aliyekuwa mwenyekiti wa NLC, Dkt Mohammed Swazuri alisema Halmashauri ya Ustawi wa Eneo la Kerio (KVDA) inayosimamia utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer, haikutoa majina ya mashamba hayo.
Utoaji kandarasi ya ujenzi ya mabwawa hayo yatakayogharimu Sh63bilioni unachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), kufuatia madai serikali ililipa Sh21 bilioni kabla ya kazi kuanza.