Habari Mseto

Naam, nataka jengo jipya wafanyakazi wangu wahudumu kwa ustaarabu – Gavana Wanga

June 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA GEORGE ODIWUOR

GAVANA wa Homa Bay Gladys Wanga ametetea uamuzi wa serikali wa kujenga makao makuu mapya licha ya kuwa na majengo mengine yanayotumika kama makao makuu.

Gavana huyo alisema afisi hizo mpya zitaimarisha shughuli za utoaji huduma kwa wakazi huku zikipiga jeki maendeleo katika maeneo ya karibu na mahala ambako majengo hayo mapya yanajengwa.

Gavana Wanga aliibua wazo la ujenzi wa makao makuu mapya baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Alidai kuwa afisi ambazo zilikuwa zikitumika na mtangulizi wake Cyprian Awiti, hazina nafasi tosha ya kuwaruhusu wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Baada ya kuingia mamlakani, Bw Wanga alihamia jengo lenye orofa nne lakini baadaye akadai halina nafasi ya kutosha.

“Baadhi ya maafisa wa kaunti wanakabiliwa na changamoto ya kupata nafasi ya kuendeshea kazi. Jengo hilo jipya litatoa mazingira bora kwao kufanya kazi,” gavana huyo akasema.

Bi Wanga alizindua ujenzi wa makao makuu hayo mapya katika eneo la Arujo Ijumaa wiki jana.

Jengo hilo ambalo litajengwa kwa mtindo wa kisasa, linatarajiwa kutumika na wanafanyakazi 1,000 na litakuwa na ukumbi mkubwa wa mikutano.

Pia jengo hilo litakuwa na kitengo cha akina mama kunyonyesha watoto, kituo cha huduma, kitengo cha serikali, afisi za idara, afisa za Bodi ya Utumishi wa Umma na idara nyinginezo za serikali ya kaunti ya Homa Bay.

“Afisi hizo mpya zitaimarisha utendakazi wa serikali ya kaunti na hivyo kuhudumia vizazi vya sasa na vijavyo,” Bi Wanga akasema.

Ujenzi wa jengo hilo unaendeshwa kwa ushirikiano na Hazina ya Pensheni katika Kaunti (CPF) na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).

Asasi hizo mbili ziliidhinisha ombi la serikali ya kaunti ya Homa Bay la kukodisha ardhi ambako afisi hizo mpya zitajengwa.

Hazina ya CPF itafadhili ujenzi huo ndani ya miezi saba kabla ya serikali ya kaunti kuanza kulipia gharama ya mradi huo kwa mfumo wa awamu ndani ya miaka 30.

Kulingana na gavana huyo, serikali ya ilifuata taratibu zote za kisheria kabla ya kufikia hazina ya CPF kwa usaidizi.

“Tulishauriana na Hazina ya Kitaifa, Msimamizi wa Bajeti na asasi zingine kabla ya kuamua kutafuta usaidizi kutoka kwa CPF,” Bi Wanga akasema.