Habari Mseto

‘Nabii’ Mary Sinaida kuzikwa Nairobi kwa kuwa hana nyumba kijijini

Na FRIDAH OKACHI November 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NABII Mary Sinaida Akatsa almaarufu Dada Mary ambaye ni mwanzilishi wa Kanisa la Jerusaleum Church of Christ atazikwa nyumbani kwake katika mtaa wa Kawangware 56, eneo bunge la Dagoretti Kaskazini, kwa mujibu wa wosia aliouandika.

Akatsa aliaga dunia Oktoba 26, 2024 katika hospitali moja jijini Nairobi, alipokuwa akipokea matibabu ya figo baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa kamati ya mpangilio wa mazishi, Bw Ezekiel Asava alisema ibada ya mwisho ya Dada Mary itafanyika Novemba 16, mtaani Kawangware.

Bw Asava ambaye ni mmoja wa viongozi ambao walilinda mali ya nabii huyo eneo la Lugari, pia, alisema sababu inayochangia kuzikwa Nairobi, muda hautawaruhu kujenga nyumba nyingine nje ya Nairobi.

“Mama aliwacha mambo yake hapa. Na alitaka sana siku atakayofariki aweze kuzikwa hapa, kijijini hakuna nyumba” alieleza Bw Asava.

Mwenyekiti wa mpangilio wa mazishi ya Akatsa katika kanisa la Jerusalem Church of Christ, Kawangware. Picha|Fridah Okachi

Mwaka wa 1988 Akasta aligonga vichwa vyombo vya habari baada ya kumleta jamaa mwenye asili ya Kieshia mtaani Kawangware akimtaja kuwa yesu, hali ambayo ilipata ukosoaji mkali kutoka kwa watu wengi.

Francis Kirato, mfuasi wa zamani, anasema yesu huyo bandia alikuwa mwenye kimo kirefu, alitembea miguu tupu na kuvalia mavazi meupe na kufunga kitambaa kwenye kichwa chake.

“Tulipaza sauti zetu na kumuita Yesu wa Nazareti. Yesu wa Nazareti tumekuja, kukuomba utuondolee dhambi zetu,” alitabasamu Bw Kirato.

Nje ya kanisa la Jerusalem Church of Christ, Kawangware. Picha|Fridah Okachi

Wafuasi hao walitangamanao na yesu huyo katika mikutano ya kanisa, iliyofanyika siku ya Jumatano, Ijumaa na Jumamosi. Bw Kirato alisema yesu huyo bandia alizungumza nao Kiswahili fasaha.

Baada ya muda wa mwezi mmoja hivi aliondoka. Mwaka wa 2000, nabii huyo alivutia ukosoaji mwingine baada ya kuwaadhibu washirika wake wa kiume kwa kiboko au kupiga magoti nje ya kanisa.

Baadhi ya wanandoa walijutia kwa kuwabeba wake wao mgongoni huku wengine wakimsifia kwa kukemea uzinzi.

Bw Zacharia Olouch, anajutia kuandamana na mkewe kutafuta ushauri wa ndoa kutoka kwa nabii.

“Nilijichukia mbona nikaenda kutafuta amani ya ndoa yangu. Baada ya kupiga magoti na kuomba msamaha mbele ya mke wangu. Kisha nikaamurishwa kumbeba mgongoni.”

Ndani ya kanisa la Jerusalem Church of Christ, Kawangware. Picha|Fridah Okachi

Hii ikiwa ni kinyume na Chrisptopher Abenzi, ambaye amesalia kuwa mjane kwa miaka 25 sasa baada ya mkewe kufariki. Bw Abenzi anasema kuwa ndoa yake ilipatwa na dosari ambayo nabii huyo hakufurahia.

“Mke wangu alikanywa kuwa na jicho la nje. Tulifanya mikutano kadhaa bila kubadilika. Siku moja Nabii alimweleza kuwa atafariki chini ya miezi miwili, hivyo nikampoteza,” alihuzunika mfuasi huyo.

Pia, aliwatia uwoga wafuasi wake katika sherehe za maziko. Bw Brian Omunzi alisema alizuru katika eneo lililo na maziko, shughuli zote zilisimama.

“Wakati wa ziara zake za mazishi, shughuli za masomo, uuzaji na ununuzi zilisimama,” alisema Bw Omunzi.