Nafasi za kazi zaendelea kuwa adimu kampuni zikifunga baadhi ya matawi
Na MAGDALENE WANJA
JUMA lililopita, kampuni ya Betin ilitangaza mpango wake wa kufunga maduka 500 kote nchini ikiwa na maana Wakenya 2,500 huenda wakapoteza nafasi zao za kazi.
Idadi hiyo ya wafanyakazi inajiunga na zaidi ya watu 2,000 ambao wamepoteza kazi tangu mwezi Julai.
Matukio hayo yamesababisha hofu kwa watu wanaofanya kazi katika mashirika mbalimbali wanaohofia kupoteza kazi zao.
Hali huenda ikawa mbaya zaidi kwani serikali imetangaza kupigwa marufuku kwa uagizaji wa bidhaa za kielektroniki ambazo si mpya kwanzia Januari 2020.
Kulingana na mkurugenzi wa elimu ya mazingira katika Wizara ya Mazingira Bw Ayub Macharia, Kenya imekuwa ikitumika na mataifa mengine yaliyoendelea kama dampo la kutupa vifaa vikuukuu vya kielektroniki.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwafanya wauzaji wa vifaa vya kielektroniki kama vile runinga, redio, friji na kebo za umeme kuwajibika zaidi.
Hii ni kutokana na sheria itayowekwa ambapo unaponunua kifaa chochote cha kielektroniki, unakatwa pesa ambazo utarejeshewa utakapokirejesha wakati kitakapoharibika.
Kulingana na mkurugenzi a kampuni ya Electronic Equipment Centre (WEEE), Bw Boniface Mbithi, Kenya hutupa taka za kielektroniki za tani 44,000 kila mwaka.
Takataka hizi huchafua mazingira kwa kiwango kikubwa.