Habari MsetoSiasa

Naibu Gavana adai wakosoaji wataka kulipwa ili wanyamaze

May 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Gitonga Marete

NAIBU Gavana wa Meru Titus Ntuchiu, Jumapili amesema wanaokashifu utawala wa Gavana Kiraitu Murungi wamekuwa wakizidisha mashambulizi yao kutokana na kunyimwa pesa na utawala wa kaunti.

Bw Ntuchiu (pichani) alidai wapinzani wa Bw Murungi walikuwa wameitaka uongozi wa kaunti uwalipe ili wakome kukosoa utawala wake lakini akasema walikasirishwa baada ya kukosa ‘kupewa kitu kidogo’.

“Tumeamua kwamba hakuna atakayepokea senti zozote zinazofaa kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ya watu wa Meru. Waendelee kupiga kelele lakini hatutashawishika kamwe kuwalipa ili wanyamaze,” akasema Bw Ntuchiu.

Mbunge wa EALA Mpuri Aburi amekuwa mkosoaji mkuu wa Bw Murungi, akimlaumu kwa kuelekeza miradi yote ya maendeleo katika eneo la Imenti na kutelekeza maeneo mengine.

Bw Ntuchiu pia alimtaka Seneta Mithika Linturi kupata habari kutoka kwa kaunti kabla ya kuibua madai yasiyo na msingi kuhusu matumizi ya fedha.